Na: Godfrey
Msinjili
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Mashariki imewataka
wananchi kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa
unaotolewa kupitia vyombo mbalimbali ili kuchukua tahadhari pale inapohitajika.
Wito huo umetolewa Februari 7, 2024 na Meneja wa Mamlaka hiyo Bi. Hidaya Senga wakati akizungumza na SUA Media ofisini kwake kuhusu mwenendo wa mvua kwa Kanda hiyo na umuhimu wa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika misimu tofauti.
Bi. Senga amesema wananchi wanatakiwa kufuatilia
taarifa mbalimbali za utabiri zinazotolewa kwa saa 24, taarifa za wiki, siku
kumi kumi na taarifa za kila mwezi ambapo kila taarifa ina umuhimu wake.
“Kwa hiyo pamoja na utabiri ule mkubwa unaotolewa
lakini ni vizuri kufuatilia taarifa za kila siku kwani zinaweza kukuokoa na
kukusaidia usifikwe na madhara yanayotokana na mvua hizi”, amesema Bi. Senga
Akizungumzia kuhusu hali ya mvua kwa mkoa wa
Morogoro amesema maeneo ya Kaskazini ambayo yanapata mvua katika misimu miwili
yaani msimu wa Vuli na Masika tayari mvua za vuli zimemalizika na kutakuwa na
upungufu wa mvua kwa mwezi Februari kama ilivyotabiriwa hapo awali lakini
wanatarajiwa vipindi vya mvua kuongezeka mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema kwa maeneo ya Kusini mwa Morogoro ambayo
yanapata mvua kwa msimu mmoja, mvua hizo zinaendelea kunyesha na utabiri
unaonesha kuwa mvua hizo zilizoanza mwezi Novemba mwaka jana zitaendelea hadi
mwezi April, 2024 ,
“Kama ilivyotabiriwa mwaka jana mvua hizo
zinaendelea kunyesha na baadhi ya maeneo mvua hizo zimeambatana na ngurumo
lakini maeneo mengine zinanyesha mvua za kawaida”, alisema Meneja huyo wa Hali
ya hewa Kanda ya Mashariki.
0 Comments