Na: George
Alexander
Wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) wamegundua mfumo mpya ambao utawawezesha wakulima na wafugaji wa
kuku kupata masoko na kuuza kwa njia ya mtandao na kuwafikia watu wengi zaidi
kwa urahisi.
Akizungumzia namna ya ufanyaji kazi wa
mfumo huo Dkt. Sixbert Mourice ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Mimea
Vipando na Kilimo Bustani amebainisha kuwa mfugaji ataweza kupakua mfumo huo uliopo
kwenye playstore ujulikanao kama E
Kuku kwenye simu yake janja ya mkononi na kujiunga kwa ajili ya kuweza
kuuza mayai na kuku kwa nchi nzima kwa urahisi.
Amesema mfugaji atapaswa kujisajili kwa
namba ya simu ambayo imesajiliwa na ataingizwa kwenye mfumo ili aweze kuingiza
bidhaa zake, na bidhaa hizo zitadumu kwa saa 24 baada ya huo muda bidhaa
zitaondoka, hivyo itampa nafasi ya kuhariri baada ya kila saa 24 hii ni
sambamba na kwenda na mabadiliko ya bei ya kila siku.
Pia ameongeza kuwa itarahisisha kwa
mnunuaji kujua bei ya Mayai au Kuku kwa urahisi na kuepusha udanganyifu na
usumbufu wakati wa ununuaji, na pia kupata bidhaa hiyo kwa urahisi kwa
kumuwezesha mnunuaji kumfikia mzalishaji bila kupitia mtu mwingine wa kati.
Amebainisha kuwa kupitia mfumo huo
kutakua na jukwaa maalum la mafunzo ambapo mtumiaji atajifunza vitu vingi juu
ya ufugaji na utunzaji wa Kuku ikiwemo namna ya kuandaa mabanda na kukabiliana
na magonjwa mbalimbali.
Hata hivyo kutakuwa na suala la Takwimu
hivyo itaonesha bei ya bidhaa kwa kila wilaya ambapo kutakuwa na bei ya juu,
bei ya chini, na bei ya wastani hivyo itampelekea mkulima kujua na kuuza bidhaa
kwa bei ya usawa na sio kuuza kwa bei ambazo sio za kweli au sio za wakati huo,
pia takwimu hizo zitasaidia pia kwenye tafiti mbalimbali.
Aidha ameeleza mfumo huo ni rahisi na
ni rafiki kwa watumiaji, na kuwa wamehakikisha habari zote za Tanzania kuhusu
masoko zitaonekana kuanzia Mkoa,Wilaya,Tarafa hadi ngazi ya chini hivyo
amewataka wakulima kuchangamkia fursa hiyo kwa maana biashara sasa inahamia
mtandaoni, na mfumo huo utatumika kama duka.
“Sekta ya Kilimo masoko yake
yanayumbishwa sana na sio ya uhakika ndio maana wakulima wengi sio matajiri
hivyo tukaangalia ni nini teknolojia inaweza ikasaidia kuhakikisha kwamba
mkulima anapata masoko, hawayumbishwi
wanakuwa na uhakika ndio tukabuni huu mfumo ili uwasaidie hawa wakulima”,
amesema Dkt. Sixbert.
0 Comments