Na: Tatyana Celestine
Ili kuhakikisha mbegu
itakayomfikia mkulima inakuwa bora na yenye tija kwa mkulima Taasisi ya
Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imekuwa ikithibitisha na kudhibiti mbegu kwa
asilimia 100 katika hatua mbalimbali.
Akizungumza katika
warsha ya mafunzo kwa waandishi wa habari mtoa mada ambaye ni Mkaguzi wa
Serikali wa mbegu kutoka TOSCI Bw. Joseph
Ngura amesema kuwa mbegu zote zinazozalishwa na kutoka nje ya nchi lazima
zithibitishwe na TOSCI na hii inawapa nafasi ya kuangamiza mbegu ambazo hazina
ubora zinazoingia nchini pamoja na zile zinazozalishwa.
Amezitaja baadhi ya
hatua ambazo mbegu hizo hupitia ni pamoja na kupimwa ubora wake, kuhakikisha
inaishi kwa muda mrefu, kuhakikisha mbegu haijachakachuliwa na kuhakikisha inawekwa
nembo ya ubora kutoka mamlaka iliyoidhinishwa na Serikali TBS.
Aidha ameongeza kuwa
wakulima wanatakiwa kutambua wana haki katika kununua mbegu na anatakiwa
akipata changamoto afuate utaratibu ili changamoto yake iweze kutatuliwa kama
vile, mbegu kushindwa kuota, kuuziwa mbegu ilyopita muda wake, mbegu iliyooza
pamoja na mbegu iliyozalishwa chini ya kiwango.
Kwa upande wake Mkaguzi
kutoka TOSCI Morogoro Bi Nugwa Fortunatus amesema kuwa wauzaji wa mbegu, miche
ya matunda wote ni lazima wapate mafunzo na wasajiliwe TOSCI ili waweze kuuza kwa
wananchi .
Akizungumza suala la
bei ya mbegu kuonekana ni kubwa kwa wakulima, Bi. Fortunatus amesema kuwa
Serikali ya Tanzania ipo bega kwa bega na tayari imetoa bei elekezi ya mbegu
kote nchini pamoja na kuendelea kufanyia kazi hata mkulima mdogo kabisa aweze
kumudu bei elekezi apate mbegu bora.
Mafunzo hayo
yamehusisha wanahabari Mkoani Morogoro ambao wamepata mafunzo kuhusiana na
uthibiti na udhibiti wa mbegu bora ili kusaidia mkulima kufahamu haki zake na
namna ya kupata mbegu bora kwa ajili ya kilimo.
0 Comments