Na; Adam
Maruma
Zaidi
ya wafugaji 40 kutoka mikoa 8 ya Tanzania Bara wamenufaika na mafunzo ya
ufugaji bora wa kuku yaliyoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa ufadhili ya mradi wa
Mabadiliko ya Elimu ya Juu Kiuchumi (HEET).
Mafunzo hayo ya siku 4 ni muendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Taasisi hiyo kwa Wakulima nchini, ambao wamekuwa wakinufaika na elimu inayotolewa kwa muda mfupi kwa makundi ya wakulima na wafugaji ili kuweza kufuga na kulima kitaalam na kuweza kunufaika na shughuli hizo kama sehemu ya kuwaongezea kipato.
Leokadia
Mhapa ni mmoja wa washiriki wa mafunzo kutoka mkoa wa Morogoro amesema mafunzo
hayo yatamuongezea maarifa zaidi kwa sababu wameanzisha kikundi cha ufugaji wa kuku kwa siku za karibuni hivyo mafunzo hayo yatawasaidia
katika mradi wao wa ufugaji wa kuku.
‘’Kwa kweli Mafunzo haya yatatusaidia sana kwa
sababu mradi wetu wa ufugaji kuku ndio kwanza umeanza, nimejua namna ya kuwapa
chanjo, namna ya kuwalisha na ujenzi wa mabanda bora, kwa kweli mafunzo haya
yamekuja kwa wakati muafaka na tunaishukuru SUA kwa mafunzo haya’’, amesema
Leokadia.
Mshiriki
mwingine kutoka wilaya Gairo Peter Kihiyo amesema mafunzo hayo yamemuongezea
uelewa wa usimamizi wa ufugaji kuku kwa sababu katika kuhakikisha usalama na
upatikanaji wa chakula kwa wananchi, ufugaji wa kuku ni eneo muhimu katika
kuwapatia wananchi protini, hivyo ufugaji wa kuku ni tasnia muhimu ndio maana
yeye na wenzake wakaamua kuja kuongeza elimu zaidi ya ufugaji kuku.
‘’Nimekuja SUA na wenzangu kwa ajili ya mafunzo ya
ufugaji bora wa kuku na hivyo uelewa wa usimamizi wa ufugaji wa kuku umeongezeka
kwa sababu katika kilimo tunachokifanya Gairo kinachosimamiwa na Kanisa la KKKT
ili kuwahakikishia wananchi usalama wa Chakula, ufugaji wa Kuku ni eneo mojawapo la mradi wetu muhimu sana kwani
inawapatia wananchi Protini pindi wanapotumia kitoweo cha kuku na hivyo mimi na
wenzangu 4 tupo hapa ili kunufaika na elimu ya ufugaji bora wa kuku na hivyo
tutakaporudi Gairo basi faida itaonekana’’, amesema Kihiyo.
Kwa
upande wake Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Dkt. Winfred Mbungu amesema katika
utekelezaji wa mradi huo, kuna maeneo 7 yanayotarajiwa kupitiwa na mradi huo,
na eneo mojawapo ni ushirikiano kati ya vyuo vikuu na taasisi binafsi na vyuo
hivyo, SUA wameamua kuendelea kuwaelimisha
wafugaji na wamekuwa wakifanya shughuli hiyo kwa muda mrefu na hivyo kwa sasa
ni zamu ya wafugaji wa kuku ili waweze kufuga kisasa na kibiashara ikiwa ni muendelezo
wa ufadhili wa mradi wa HEET.
Nae
mwezeshaji wa mafunzo hayo Prof. Faustine Lekule, ambae ni Prof. mstaafu kutoka
Idara ya Sayansi ya Wanyama SUA, ameupongeza mradi wa HEET ambao ndio
wawezeshaji wa mafunzo hayo na kusema kitendo cha washiriki wa mafunzo hao
kutoka mikoa 8 inaonesha mwamko wa watanzania kutaka kujifunza mambo mapya
katika ufugaji wa kuku nchini.
Aidha
Prof. huyo mbobezi wa masuala ya Sayansi ya Wanyama ameongeza kuwa ufugaji kuku
ni tasnia ambayo mfugaji anaweza kuanza kidogo kidogo na hivyo hata mfugaji
mdogo anaweza kuifanya shughuli hiyo na kufuga kwa tija na kuweza kumuinua
kiuchumi.
Kwa
mujibu wa takwimu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Tanzania inakadiriwa kuwa na
idadi ya kuku milioni 92.8, kuku wa asili wakikadiriwa kuwa milioni 42.7 na
kuku wa kisasa wakiwa milioni 50.1, hata hivyo kutokana na wafugaji wengi
kufanya shughuli hiyo kimazoea imekuwa na mchango mdogo katika kuchangia pato la
wafugaji na taifa kwa ujumla kutokana na changamoto ya maradhi yanayochangiwa
na ukosefu wa elimu.
0 Comments