Nal: Ayoub
Mwigune
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Kurugenzi ya
Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam kwa siku
mbili mfululizo kimeendelea kufanya mapitio ya Programu zao za Shahada za
Uzamili kwa lengo la kuziboresha ili ziwe na uwezo wa kuyafikia mahitaji ya
jamii ya watanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Japhet Kashaigili wakati akizungumza na SUA Media ambapo amesema wamekuwa wakifanya mapitio hayo ya Mitaala chini ya Program ya HEET ambayo imewawezesha kuangalia Mitaala yao iko kwenye hali gani kwa sasa ukilinganisha na uhalisia wa soko ili waweze kuiboresha na kufikia matakwa ya soko ambapo ni jambo la msingi katika kuleta manufaa yenye tija.
Amesema mapitio hayo yamefanywa na wataalam wa Chuo lakini
pia yamewahusisha wadau mbalimbali ambao ni wanafunzi waliohitimu Chuoni hapo,
wadau kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali pamoja na za umma na watu binafsi
ambao wanavutiwa na program zinazotolewa na SUA na kwamba zoezi hilo ni la
msingi kwa kuwa linawawezesha kujua aina ya program walizonazo na zinahitaji
nini ili kuweza kuwa na mvuto zaidi na hivyo kuweza kupata wanafunzi wengi
kwenye Chuo hicho.
"Kwa hiyo hili ni zoezi muhimu sana kwa sababu linaonesha
mustakabali wa Chuo kwa maana ya kwamba wanafunzi ambao watakuja chuoni kwetu
lakini pia matumizi ya wale wahitimu wetu ni wapi wanaweza wakaajiriwa hivyo
suala hili linaandaliwa kwa ajili ya kujenga maendeleo ya ujuzi kwenye suala
zima la uandaaji wa hizi program ambazo tumekuwa tukiendelea kuzipitia”,
alisema Prof. Kashaigili.
Aidha amesema licha ya kufanyia maboresho program zilizo kuwepo
vile vile wanaanzisha program zingine mpya kulingana na hitaji la soko kwa sasa
ikiwemo kuingiza masuala ya namna ya kutumia akili bandia (Artificial
Inteligency) kwenye masuala ya uzalishaji na masuala mtambuka ambayo yanaendana na soko la sasa.
Kwa upande wake Dkt. Zahra Majili amesema wanacholenga
ni kuhakikisha Mitaala yao inaweza kuendana moja kwa moja na soko la ajira
lakini pia hali halisi ya muhitimu anayetoka SUA kuweza kuwa na uwezo wa kupata
kazi kwa haraka iwe kwa kuajiriwa au kujiajiri hivyo wanahitaji elimu ambayo itawafanya
wadau wao ambao ni wanafunzi iweze kuchangia katika kuhamasisha ukuaji wa
uchumi wa nchi.
Naye mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika zoezi hilo Rafiki
Hamza amesema kuwa manufaa makubwa ya zoezi
hilo ni kuwa Mitaala hiyo inalenga kutengeneza wahitimu watakaoenda kuuzika
kwenye soko la ajira wakiwa na ujuzi ambao unahitajika kuendana na mabadiliko
ya Kiteknolojia lakini pia mifumo ya kijamii.
0 Comments