Na: Adam Maruma
Vijana mkoani Morogoro
wametakiwa kuiangalia tasnia ya ufugaji Kuku kama shughuli inayoweza kuwa
suluhisho la tatizo la ajira nchini kutokana na urahisi wa kuanzisha mradi huo
na kupata faida ndani ya muda mfupi tangu mradi kuanza.
Hayo yameelezwa na Shomari Mtandu ambaye ni mmoja wa wafugaji waliofanikiwa kutokana na ufugaji katika tasnia ya ufugaji kuku katika kata ya Kingolwira baada ya kutembelewa na washiriki wanaofanya mafunzo ya ufugaji bora wa kuku yaliyoandaliwa naTaasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kwa ufadhili wa mradi wa Mabadiliko ya Elimu ya Juu Kiuchumi (HEET).
Mfugaji huyo amesema ufugaji wa
kuku ni tofauti na shughuli zingine ambazo mchakato wa uanzishwaji huwa na
mlolongo mrefu, lakini ufugaji wa kuku kinachotakiwa ni eneo na baadhi ya vifaa muhimu na unaweza kuanza na kiasi
chochote cha kuku huku ukiendelea kujifunza na kukuza biashara na matokeo huwa
ni muda mfupi kwani kuku wa nyama wanaweza kuwa tayari kuuzwa baada ya wiki 4.
‘’Ufugaji
kuku ni tofauti na shughuli kama duka la mahitaji ya nyumbani kwani utahitaji
vitu vingi, kama leseni na kodi na mambo mengine, kwa ufugaji wa kuku kikubwa
ni eneo na kuku wenyewe na mahitaji mengine ambayo hutegemeana na aina ya kuku
na idadi ndio maana kuna watu wameanza na kuku 10 na sasa wana idadi kubwa sana
ya kuku’’, amesema Shomari.
Ameongeza kuwa shughuli hiyo
amekuwa akifanya kwa muda mrefu kwani wazazi wake ndio waanzilishi na yeye
akajikuta anaungana nao baada ya kuona manufaa kutokana na ufugaji huo ambao
kwa sasa wamekuwa wakiuza mayai na nyama jijini Dar es Salaam kwa kuwa ana miliki
kuku zaidi ya 2,000 kwenye mabanda yake wenye ukubwa tofauti.
Kwa upande wake mfugaji mwingine,anayejulikana kama Mama Ado ambaye
pia ana mradi wa ufugaji kuku amesema pamoja na changamoto za bei kubwa
ya chakula cha kuku, lakini amemudu kuendesha maisha ya familia yake kutokana
na ufugaji huo, na ameshukuru kwa kutembelewa na wafugaji wengine kwani
imemuongezea ari ya kujituma zaidi katika ufugaji kuku.
‘’Ufugaji
kwa siku za mwanzo unakuwa na changamoto hasa kwenye chakula cha kuku kwani bei
zinakuwa kubwa na kama utakuwa huna elimu ya namna ya kuwalisha vizuri, unaweza
kujikuta unapata hasara sana lakini nimefurahi kwa ugeni huu wa wafugaji hawa,
imeniongezea ari zaidi ya kufuga na siku nyingine mkija mtanikuta na idadi
kubwa zaidi ya hawa, nawashukuru SUA kwa kuchagua eneo langu kama sehemu ya
kujifunza kivitendo’’, amesema mama Ado.
Kwa mujibu wa Dk. Juma Yusuph
ambaye ni mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Kata ya Kingolwira ni miongoni
mwa kata iliyo na mwamko wa ufugaji kuku huku kata hiyo ikiwa na zaidi ya
wafugaji 25 ambao wanafuga katika maeneo wanayoishi na amekuwa akiwatembelea na
kuwapa huduma za ugani.
0 Comments