Na: Farida Mkongwe
Rai imetolewa kwa vyombo vya
habari nchini kuwa na vipindi maalum vitakavyohamasisha jamii kuzijua mila na
desturi za kitanzania ili kujenga taifa lenye maadili na uzalendo ambao ndio
chachu ya maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa Februari
13, 2024 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Mhandisi Kundo Mathew wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji
nchini ikiwemo unaofanyika jijini Dodoma.
Mhandisi Mathew amesema pamoja
na mafanikio makubwa yanayotokana na uwepo wa vyombo vya habari kuweza kuifikia
jamii kirahisi zaidi lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya vyombo hivyo
kukiuka kanuni za utangazaji hali inayochangia kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili
nchini.
“Sekta ya habari imekumbwa na mabadiliko ya
Teknolojia na hivyo kuathirika na utandawazi uliopo, sisi sio kisiwa lakini
pamoja na hayo Serikali inaendelea kufuatilia na kuchukua hatua stahiki ikiwa
ni sanjari na kutoa elimu kwa vyombo hivyo ili kukabiliana na changamoto
zinazotokana na mabadiliko hayo ya teknolojia”, amesema Mhandisi Mathew.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri huyo amewataka washiriki waliohudhuria mkutano huo kuzielewa ipasavyo Kanuni
za uchaguzi zinazotumika nchini ili uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa
kufanyika mwishoni mwa mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani
uwe wa amani na mafanikio makubwa.
Miongoni mwa mada
zinazojadiliwa katika mkutano huo ni Hali ya Maadili na Matumizi ya Taaluma ya
Utangazaji nchini, Hali ya Maadili na Matumizi ya Taaluma ya Utangazaji kwenye
mitandao ya kijamii, Matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa watengeneza
maudhui, pamoja na matumizi ya kazi za Sanaa na Filamu kwenye vyombo vya
Utangazaji.
SUA Media imeshiriki katika Mkutano
huo unaofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma ambao umebeba Kauli Mbiu isemayo “
Maadili na Taaluma ya Utangazaji".
0 Comments