SUAMEDIA

SUA yashiriki Maadhimisho ya Kitamataifa ya Siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi

 Na George Alexander

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeshiriki katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika Sayansi, ambayo kitaifa imeadhimishwa katika Mkoa wa Arusha na mgeni rasmi akiwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolijia Mheshimiwa Prof Adolph Mkenda.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolijia Mheshimiwa Prof Adolph Mkenda akihutubia katika mkutano wa kimataifa wa siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi (Picha na George Alexander)


Mheshimiwa Prof Mkenda katika hotuba yake amewaasa wasichana kujikita zaidi kwenye masomo ya sayansi na kuwahakikishia kuwa serikali ipo sambamba katika kuhakikisha wanapata elimu bora.

Ameongeza kuwa ulimwengu wa sasa umebadilika na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanakuwa kwa kasi pia, hivyo kama taifa linahitaji zaidi wasomi wa Sayansi na hivyo litaendelea kuwapatia motisha wanafunzi ili wapende kusoma masomo ya Sayansi, na wanaohitimu kupata fursa zaidi kutoka serikalini mfano Samia Scholarship ambayo serikali imekuwa ikiitoa kwa wanafunzi wanaofaulu masomo ya Sayansi.

Aidha Prof. Mkenda amewataka wahadhiri wa vyuo kuwa walezi bora kwa wasichana na sio kuwa sababu ya kuwakatisha ndoto zao, hivyo kama serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wahadhiri watakapogundulika kuwa ni sababu ya kumkwamisha msichana.

Naye Mkuu wa Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji na pia Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA Dkt. Hadija Mbwana ameeleza kuwa SUA inaendelea kutoa nafasi kwa wasichana wa wanawake katika uongozi kwa kutoa kipaumbele kwenye nyadhifa za uongozi.

Mkuu wa Idara ya Lishe na Sayansi ya Mlaji na pia Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA Dkt. Hadija Mbwana aliyevaa hijabu mbele akisikiliza hotuba ya mgeni rasmi

Ameongeza kua kwa upande wa wanafunzi wa kike wamekua wakiwapatia kipaumbele kwa kuwapa hosteli waingiapo chuoni. Lakini pia kuanzisha dawati la jinsia kwa lengo la kutoa uhuru na nafasi kwa wasichana na wanawake kupeleka malalamiko yao mbalimbali.

Maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Wanawake na wasichana katika uongozi wa Sayansi enzi mpya na maendeleo endelevu’ yamehudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka vyuo vikuu na vyuo vya kati, pamoja na wasichana mbalimbali kutoka katika shule za sekondari na msingi. lengo ni kumjenga mwanamke na msichana katika Sayansi na teknolojia.

Maadhimisho hayo yametanguliwa na maonesho mbalimbali ya kisayansi kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini pamoja na shule za sekondari, na Chuo Kikuu cha Kilimo SUA kuwa sehemu ya maonesho hayo ya Kisayansi kwa kupitia wataalam wake.




Post a Comment

0 Comments