Na: Gerald Lwomile
Imeelezwa kuwa ushirikiano ulioanzishwa
kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu cha Artemisa cha
Jamhuri ya Cuba utakuwa na manufaa makubwa baina ya vyuo vikuu hivyo kwani
utainua taaluma, ujuzi na kunufaisha wananchi wa pande zote mbili yaani
Tanzania na Cuba.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda akimpa zawadi ya kalenda Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Artemisa Dkt. Adianez Bermundes (Picha na Ayoub Mwigune) |
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa Manejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Januari 25, 2024. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Artemisa Dkt. Adianez Bermundes amesema mahusiano baina ya pande hizo mbili yatawajengea uzoefu, ujuzi na taaluma wanafunzi na wanataaluma kwa kubadilishana uzoefu, teknolojia na kufanya utafiti mbalimbali.
Ametolea mfano mazao ya mihogo,
viazi na magimbi kuwa ni baadhi ya mazao ambayo yamefanyiwa na yanaendelea
kufanyiwa tafiti katika Chuo Kikuu cha Artemisa ili kuona ni kwa namna gani
watu wanaweza kuendelea kuyatumia huku wakichanganya na vyakula vingine ili
kuondoa hali ya kutegemea kula chakula cha aina moja.
Akizungumzia namna ya kuinua hali
za wakulima katika maeneo ya nchi Dkt. Bermundez amesema chuo chao kimekuwa
kikitoa elimu ya moja kwa moja kwa wazalishaji wa mazao jambo ambalo limekuwa
na mafanikio makubwa pamoja na kuwa nchi yao imekuwa katika vikwazo mbalimbali kwa
muda mrefu lakini imejimudu kwa kuwa na chakula cha kutosha.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Artemisa Dkt. Adianez Bermundes wa pili (kulia) akisikiliza maelezo ya namna ya kutibu wanyama katika Hospitali ya Rufaa ya Wanyama iliyopo SUA. |
Katika hatua nyingi ametoa ahadi
kwa SUA kuwa atakiunganisha chuo hicho na vyuo vingine vinavyotoa elimu inayolingana
na ile wanayoitoa SUA ili kuleta ufanisi zaidi kwa Tanzania lakini pia kwa Cuba.
Awali akimkaribisha Dkt.
Bermundez Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael
Chibunda amesema Januari 24, 2024 SUA na Chuo Kikuu cha Artemisa vilitia saini Hati
ya Makubaliano baina ya pande hizo mbili mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Mungano wa Tanzania Mhe. Philipo Mpango na Makamu wa Rais wa Cuba Mhe Salvador Veldas Mesa .
Aidha Prof. Chibunda amemshukuru
Dkt. Bermundez kwa kukubali kualika ujumbe kutoka SUA kwenda nchini humo mapema
mwaka huu ili kuona ni kwa namna gani pande hizi mbili zitanufaika na
ushirikiano huo.
Aidha Dkt. Bermundez alipata
wasaa wa kujua mambo mbalimbali yaliyopo SUA ambapo katika wasilisho
lake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof.
Maulid Mwatawala amesema chuo kimekuwa na mafanikio makubwa tangia
kuanzishwa.
Akitoa neno la shukrani kwa ujio
wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Artemisa cha Cuba, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa
amesema ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba ni wa kihistoria na anatarajia
ushirikiano baina ya SUA na Artemisa utaleta matunda makubwa si kwa vyuo hivyo
pekee lakini kwa wanachi wote.
Akiwa Chuoni hapo Dkt. Bermundez
ametembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Wanyama
iliyopo SUA.
Matukio mbalimbali katika picha 👇
0 Comments