Na: Winfrida Nicolaus
Ndaki ya
Tiba ya Wanyama na Sayansi Shirikishi pamoja na Idara ya Sayansi ya Wanyama ya
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na wadau toka taasisi
mbalimbali nchini wameombwa kufanya maboresho ya Mitaala yatakayo muwezesha
muhitimu kutoka SUA kwenda kuwa bidhaa ya kibiashara yenye kukidhi soko la
ajira licha ya ugumu wa kozi wanazozichukua.
Hayo yamesemwa
na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam SUA Prof.
Maulid Mwatawala wakati akifungua mkutano maalumu wa wadau kutoka taasisi
mbalimbali waliokutana kufanya mapitio ya maboresho ya Mitaala iliyotengenezwa
na Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi Shirikishi pamoja na Idara ya Sayansi ya
Wanyama kwa kuangali kama inafikia malengo na matarajio ya wanafunzi wao katika
kujiajiri au katika ya soko la ajira.
Amesema kutokana
na wadau wengi kwenye soko la ajira kutegemea bidhaa zinazozalishwa na chuo hicho
ni muhimu kuangalia kama Mitaala wanayoiboresha inamuwezesha muhitimu kutoka
SUA kuajirika kwa maana ya Kozi wanazozitoa zibebe vipengele vya kibiashara
vitakavyomuwezesha muhitimu kutoka SUA kuweza kuajirika kirahisi vilevile kuhakikisha
harakati za mwanafunzi kupelekea kutimiza malengo yake na kuhakikisha ubora wa
wanachozalisha unabaki palepale.
Kwa
upande wake Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi Shilikishi SUA Prof.
Esron Karimuribo, amesema wanacholenga ni kuhakikisha Mitaala yao inaweza kuakisi
hali halisi ya muhitimu anapomaliza elimu ya Chuo Kikuu kuweza kuwa na uwezo wa
kupata kazi kwa haraka iwe kwa kuajiriwa au kujiajiri hivyo wanahitaji elimu
ambayo wadau wao ambao ni wanafunzi watakayoipata ichangie katika kuhamasisha
ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha
amesema wameamua kuleta zoezi hilo ambalo limewashirikisha wadau ili kuwapa
maoni juu ya namna ya kuboresha Mitaala hiyo na kisha wataiwasilisha kwenye
Seneti ya chuo na baadae kupata uthibiti wa Tume ya Vyuo Vikuu ili wanapoanza
kuitumia iweze kuleta matokeo chanya katika kutoa ajira pamoja na mchango
mkubwa kwenye uchumi wa nchi hivyo ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kufadhili zoezi hilo kupitia mkopo kutoka Benki ya dunia kwenye Mradi wa HEET.
Naye
Prof. Robinson Mdegela Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na
Sayansi Shirikishi, Idara ya Tiba ya Wanyama na Afya ya Jamii SUA amesema kwa
sasa chuo chao kinafanya kazi kubwa katika Mradi wa HEET wa kuhakikisha kuwa
wanakuwa na Mitaala inayojitosheleza na kujibu mahitaji ya wanafunzi wao wa
sasa na watakaokuja baadae pamoja na
waajiri na hasa inapozingatiwa kuwa wapo katika hatua ya sita kwa mapinduzi ya
viwanda nchini.
“Tuna
Mitaala zaidi ya ishirini na tatu (23) kwa upande wa Tiba ya Wanyama na Sayansi
Shilikishi na upande wa Sayansi ya Wanyama na hiyo Mitaala yetu
imetengenezwa na wataalamu wetu tulio
nao, ukitaka Mtaala uwe na Tija ni lazima uite wadau watakao kupatia mawazo ya kitu gani
kinatakiwa kufanyika ili Mitaala yetu kuuzika na kuwa maana zaidi”, alisema Prof. Megela
Aidha
amesema kumekuwa na ushirikianao mkubwa kutoka kwa wadau na wamepata ushauri mzuri
utakaowasaidia kuboresha Mitaala na kufanya vijana wao waweze kuajirika na
kukubalika katika soko la ajira lililopo nje ya chuo.
Naye
Rais wa wanafunzi wa Tiba ya Wanyama Tanzania Bw. Samwel Nyambasoba ambaye pia
ni mwakilishi wa wanafunzi wa Tiba ya Wanyama SUA amesema manufaa makubwa ya
zoezi hilo ni kuwa Mitaala hiyo inalenga kutengeneza wahitimu watakaoenda
kuuzika kwenye soko la ajira wakiwa na ujuzi ambao unahitajika kuendana na
mabadiliko ya Kiteknolojia lakini pia mifumo ya kijamii hivyo lengo la
kuhusishwa kwa wadau mbalimbali katika zoezi hilo ni kuweza kupata maoni ya
pamoja ambayo yanalenga kuleta mabadiliko kwenye sekta ya uchumi na kijamii.
Wadau
mbalimbali kutoka Sekta za Viwanda walioshiriki katika zoezi hilo la uboreshaji
wa Mitaala ni pamoja na washauri wa Sekta ya Viwanda katika ngazi ya taifa,
waajiri upande wa Sekta Binafsi pamoja na Sekta za Umma, wanafunzi wanaosoma
Shahada ya Kwanza naya Pili, wasimamizi wa mafunzo wanayoyatoa (Professionals Bodies)
pamoja na vyama vinavyoajiri wahitimu wao katika sehemu mbalimbali.
0 Comments