Na: Calvin Gwabara – Tabora.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya
Tumbaku Tanzania (TTB) Bwana Stanley Nelson Mnozya kwa niaba ya Wakulima wa Tumbaku
nchini amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa
na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Taaasisi ya Utafiti wa Tumbaku
nchini TORITA kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kuwezesha upatikanaji wa
mbegu bora za Tumbaku ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya
kumalizika kwa kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa TORITA wakati wajumbe hao
walipotembelea kuona aina mpya za mbugu bora za Tumbaku zinazojaribiwa kutoka
nchini Barazil ambazo zinauwezo mkubwa wa kuzalisha Tumbaku kuliko mbegu ambazo
wakulima wamekuwa wakizitumia kwa miaka mingi hapa nchini.
“Tumeona haya majaribio ya mbegu
mpya za Tumbaku ambayo TORITA inaendela nayo hapa Tabora, tumeona majaribio
kama matano hivi ambazo ni mbegu mpya toka nchi ya Brazil hili na jambo kubwa
sana ambalo linafanywa na Serikali yetu kwenye sekta ya Tumbaku, tunavyoona
mbegu zinazidi kuingia aina kwa aina tena kutoka nchi zinazosifika kwa kilimo
cha Tumbaku duniani inatupa moyo sana” alieleza Bwana Stanley.
Aliongeza “Kwa niaba ya Wakulima
wa Tumbaku nchini niwapongeze TORITA kwa kazi hii nzuri iliyotukuka lakini ni
kazi ambayo inaunga mkono jitihada za Mama yetu Dkt. Samia suluhu Hassan
kupitia Waziri wake wa kilimo Mhe. Hussein Bashe ambayo amekuwa akiifanya usiku
na mchana kuhakikisha sekta ya Tumbaku inatulia na wote tunaona katika miaka
miwili mitatu iliyopita tulikuwa tunaongelea uzalishaji wa tani milioni 37 za
Tumbaku nchi nzima lakini mwaka huu
2022/2023 uzalishaji umeenda hadi kilo milioni 122 na zao kuingia dola za
kimarekani zaidi ya milioni 286 kwa nchi nzima”.
Ametumia nafsi hiyo kuwaasa
wakulima kuamka na kujiandaa kwa mabadiriko makubwa katika upatikanaji wa mbegu
bora zenya tija kubwa kwakuwa Serikali hii inafanya jitihada kubwa za
kuhakikisha inawakomboa na kuwainua kwakuwa mbegu hizo walizoziona zikifanyiwa
majaribio zinafanya vizuri sana kuliko mbegu walizonazo wakulima kwa sasa hivyo
ni neema kwa wakulima wa Tumbaku nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi ya TORITA kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
Prof. Gration Rwegasira amesema kuwa mbegu hizo zinazofanyiwa majaribio kutoka
Brazil ni sehemu tu ya mahitaji ya soko lakini TORITA inazalisha aina
mbalimbali za mbegu na kuboresha zile ambazo zinatumiwa na wakulima nchini kwa
sasa lakini pia wanazalisha kulingana na uhitaji wa soko kama la Marekani, Asia
na kwingineko.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa
namna inavyoisaidia TORITA lakini tungeomba wanapoweka ruzuku katika uzalishaji
wa mbegu za mazao mbalimbali wakumbuke sana zao la Tumbaku kwakuwa halina
kampuni binafsi inayoizalisha mbegu ya Tuambaku wala Taasisi kama ASA ambao
wanazalisha na kusambaza mbegu za mazao mengine, Mbegu za Tuambaku zinazalishwa
na TORITA tu nchini.” Alifafanua Mwenyekiti wa Bodi Prof. Rwegasira.
Hivyo ameiomba Serikali inapoitikia
kwenye masuala ya mbegu iweze pia kuingalia TORITA na kuingozea fedha ili iweze
kuzalisha mbegu za aiana mbalimbali na za kutosha na kuwezesha wadau waweze
kuzipata mbegu hizo bora hapahapa nchini.
“Tunajua Serikali iliweka mkazo
kuwa mbegu za mazao mbalimbali yanayolimwa nchini zizalishwe hapa hapa ndani na
sio zitegemewe kutoka nje, jambo ambalo TORITA ililiitikia na kulifanyia kazi
kwa bidii na kuhakikisha mbegu za Tumbaku zinazalishwa hapahapa nchini na
tunaweza kusema sasa kuwa tuna mbegu za kila aina za kuwafaa wadau wote
kulingana na mahitaji ya soko hivyo Serikali itusaidie tuzizalishe kwa wingi mbegu
hizi zipatikane kwa wadau ili kufikia malengo yake ya wakulima kupata mbegu
bila vikwazo” alieleza Prof. Rwegasira.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti
wa Tumbaku (TORITA) Dkt. Jacob Bulenga Lisuma amesema kuwa kwenye jaribio hilo
la mbegu kutoka Brazil zipo za aina tatu ambazo ni AOV 12, AOV 405 na AOV 815
na zinapambanishwa na Mbegu aina ya RG 17, K326 ili kuangalia uzalishaji wake.
“Tumeshafanya majaribio kwa miaka miwili na
tumeweza kuzalisha kilo 3425 kwa hekta huu ni uzalishaji mkubwa sana, sasa
jaribio hili lipo katika awamu ya mwisho na tunafanya kwa kushrikiana na
Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na jaribio hili
likikamilika hatua za usajili zitafuta” Alifafanua Dkt. Jacob.
Amesema pamoja na uzalishaji wa
mbegu hizo kuwa mkubwa ikilinganishwa na mbegu zinazolimwa sasa na wakulima
lakini sifa nyingine kubwa ni uwezo wa mbegu hizo katika kukinzana na magonjwa
ya Minyoo fundo (nematode) ambao
wanasababisha Tumbaku kudumaa.
Aidha amesema kutokana na
ongezeko kubwa uzalishaji lililopatikana na mwaka huu kutoka tani milioni 37 za
Tumbaku nchi nzima hadi tani milioni 122
mwaka huu 2022/2023, ana imani kuwa kuanza kutumika kwa mbegu hizo mapema
wanaweza kufikia lengo walilopewa na Serikali katika sekta ya Tumbaku la
kuzalisha tani milioni 200 ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi huyo wa TORITA amesema
tayari chama kimeshamshukuru Waziri wa kilimo Mhe. Bashe kwa jitihada zake za
kufikia uzalishaji huo mkubwa kwa mwaka huu na kipande kilichobaki kwenda
kwenye tani milioni 200 kutoka kwenye tani 122 ni kitu kidogo sana na takwimu
zitaonesha namna Tumbaku inavyoiingizia nchi fedha nyingi za kigeni.
Amesema kulingana na taratibu za
usajili wa mbegu nchini mbegu hizo zinazofanyiwa majaribio zinaweza kuanza
kulimwa na wakulima mwaka 2026/2027 ila kama zitawahi kwa kufuata taraibu
zinaweza kuwafikia wakulima mwaka 2025/2026.
Dkt. Jacob ameshukuru mchango
mkubwa unaotolewa na Bodi ya wakurugenzi ya TORITA katika kutimiza malengo ya
uanzishwaji wa Taasisi hiyo na hivyo kuahidi kuendelea kusaidia lengo kubwa la
Wizara ya kilimo la Sekta ya kilimo kuweza kuchangia asilimia 10 kwenye pato la
Taifa ifikpo mwaka 2030.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku
(TORITA) Dkt. Jacob Bulenga Lisuma (wa kwanza kulia) akijibu maswali na kutoa
ufafanuzi kwa wajumbe wa bodi kwenye shamba hilo la majaribio. |
0 Comments