Na: Ayoub Mwigune
Katika kuhakikisha wahitimu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanakidhi mahitaji ya soko la ajira sambamba
na kuwa na ujuzi utakaowasaidia kuweza kujiajiri, Ndaki ya Kilimo ya SUA
imekutana na Wadau mbalimbali kutoka sekta tofautitofauti zikiwemo za Umma na
Binafsi ili kupitia na kufanya maboresho
na kukuza Mitaala yake.
Wadau mbalimbali wakiwa katika mkutano wa kuboresha Mitaala |
Akizungumza na SUA Media katika mkutano
huo Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA Dkt. Nyambilila Amuri wameona ni vyema kukutana
na wadau mbalimbali ili kuboresha na kuhuisha Mitaala hiyo ili kwenda sambamba
na mapendekezo yaliyotolewa.
Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA Dkt. Nyambilila Amuri (wa nne kutoka kushoto mstali wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wadau |
Dkt. Nyambilila amesema lengo kubwa la
kuwakusanya wadau hao ni kuweza kupata maoni na kupata mrejesho kutoka kwao ya
matarajio ya wahitimu watakaoenda kutengenezwa kutokana na Mitaala hiyo na
kudumisha ubora wa wahitimu lakini pia kuhakikisha wahitimu hao wanakidhi
mategemeo ya soko la ajira na wale watakaojiajiri ikiwa ni pamoja na
watakaoanzisha biashara kilimo.
“Tumepitia na tumeweza kupata maoni
kwenye Programu nne za Shahada za Awali……., umetuwezesha kupata maoni mazuri
ambayo yatatusaidia kuboresha Mitaalala yetu lakini zaidi ya hapo pia tuna
Mitaala ya Program za Uzamili ambazo zimejadiliwa kwenye kikao hicho zinafikia
kumi lakini pia kuna zile za Umahili pamoja na Uzamivu”, alisema Dkt.
Nyambilila.
Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji
Bw. Emanuel Mnyanye Mtumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro amesema
lengo la kukutana kwao katika uboreshaji wa Mitaala SUA ni kusikiliza na kutoa
maoni yao kwa lengo la kupata wahitimu bora watakaoweza kuwasaidia utendaji wa
kazi katika kukuza Uchumi wa nchi pamoja na uzalishaji kwa ujumla.
Amesema wameona ni vyema wakajikita
kutoka kwenye uelewa kinadharia na kwenda kwenye ujuzi ambapo utawafanya
wahitimu wengi kutoka SUA wakiwa na ujuzi ambao wataenda kuuwekeza kwa wakulima
na kupata matokeo chanya, vilevile kutoka chuoni wakiwa na uwezo wa kujitegemea
wenyewe kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi lakini pia kuajirika kimataifa.
Naye Bi. Given Msomba kutoka Chuo Kikuu
cha Iringa mmoja wa wadau aliyeshiriki katika mkutano huo wa uboreshaji wa
Mitaala ya Ndaki ya Kilimo SUA amesema imekuwa ni nia ya Serikali pamoja na
wadau mbalimbali kuwa wawe na Mitaala ambayo inakidhi kiwango cha wadau
vilevile itakayowasaidia wanafunzi kupata utaalamu wa kuweza kufanya kazi
sehemu mbalimbali ndani nan je ya nchi.
0 Comments