Na; Godfrey Msinjili
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wameishukuru Bodi ya Mikopo kwa kuwarahisishia kupata fedha za kujikimu na
matumizi kwa wakati kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
ambapo imewezesha wanafunzi hao kuendelea na masomo kwa wakati Chuoni hapo.
Akizungumza na SUA Media katika mahojiano yaliyofanyika Chuoni hapo, Mhasibu na Afisa Mikopo wa Dawati la Mikopo la Elimu ya Juu kutoka SUA Frida Malya, amesema wanaendelea na zoezi la kuwasajili wanafunzi wanufaika katika Mfumo mpya wa Kidijitali wa Malipo (Digital Disbursement Solution – DiDiS ) wakisaidiana na Maafisa kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Aidha Malya amesema kuwa mfumo huo ulioboreshwa utasaidia
wanufaika kuachana na mfumo wa kusaini pesa kwenye makaratasi badala yake watapata
fedha za kujikimu ndani ya saa 24 baada ya kutumiwa ujumbe wa kuingiziwa pesa
kutoka Bodi ya Mikopo.
Amefafanua kuwa mnufaika ataweza kutumia simu yake kupakua
fedha akiwa mita 100 kutoka Jengo la Utawala na kuongeza kuwa mfumo huo
utasaidia wanafunzi kupata mahitaji
muhimu na kupata muda mzuri wa kuendelea na masomo mapema.
Kwa upande wake Afisa Mikopo Daraja la Pili kutoka HESLB
Edward Kilele ameeleza kuwa mfumo huu wa DiDiS ni mfumo wa Kidigitali ambapo mnufaika
atatumia mfumo wa Student’s Individual
Permanent Account (SIPA) kuangalia mgawanyo, na itasaidia kupunguza adha ya foleni kwa wanafunzi, pia
itasaidia Bodi ya Mikopo kufanya ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa
wanafunzi wanaweza kupata fedha kwa kupakuwa application ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu yaani ‘HESLB App’.
"Tunaishukuru sana Serikali kwa ufadhili huu wa fedha
pia naishukuru Bodi ya Mikopo kwa kugundua mfumo mpya wa DiDiS ambao
umerahisisha kupata fedha za kujikimu na matumizi kwa urahisi tofauti na zamani
ambapo pesa zikitoka tunapanga foleni, lakini kwa sasa tunaweza kupata fedha
popote tulipo na kwa wakati, pia nawashauri wanafunzi wenzangu tutumie fedha
vizuri ili tuendelee kufaidika na ufadhili huu", alisema Albertina Kihundwa, Mwanafunzi wa Mwaka
wa Pili wa Stashahada ya Kwanza ya Udaktari wa Wanyama Chuo cha SUA.
Kwa upande wao Ruth Msechu, anayesoma Kozi ya Kilimo na Antony
Michael Kozi ya Shahada ya Uuguzi wa Wanyama wote wakiwa ni wanafunzi wa mwaka
wa pili SUA wameishukuru Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa kuruhusu mfumo huo
mpya ambao umesaidia wanafunzi kujihudumia wenyewe na hivyo kuwawezesha kuanza
masomo kwa wakati.
Mfumo huu wa DiDiS unalenga kusajili wanafunzi waliopata mkopo
kwa mara ya kwanza katika mwaka wa masomo 2022/2023 waliopo katika Taasisi zote
za Elimu ya Juu nchini, usajili utakapokamilika wanafunzi wote wanufaika wa
mikopo waliopo vyuoni wapatao 202,016
watakuwa wanapokea fedha kupitia DiDiS.
0 Comments