SUAMEDIA

KKU - SUA yawataka wanafunzi kuzikabili changamoto walizonazo pasipo kukiuka maadili

 Na: Gerald Lwomile

Mwenyetiki wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Christopher Mahonge amewataka wanafunzi wa SUA kuhakikisha wanazikabili changamoto za kimaadili wanapokuwa na hata wakiwa nje ya chuo.

Prof. Christopher Mahonge akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda (Picha zote na Gerald Lwomile)

Prof Mahonge amesema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wanafunzi wa SUA Kampasi ya Mizengo Pinda iliyoko Wilayani Mpimbwe mkoani Katavi.

Amesema ushirikiano baina ya wanafunzi, waalimu na wafanyakazi utawafanya kutegemeana na utegemeano huo unaweza kuleta matokeo chanya katika masomo yao na hata katika utendeaji wao wa kazi huku wakizingatia maadili.

Akizungumzia changamoto za kimaadili zinazowakabili wanafunzi, Prof. Mahonge amesema changamoto ni nyingi ikiwemo mavazi yasiyo na heshima, lugha chafu, utapeli, uporaji na unyang’anyi, migogoro baina ya viongozi na wanafunzi na matumizi mabaya ya fedha.

Mwenyekiti wa KKU - SUA Prof. Christopher Mahonge aliyekaa katikati akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda

“Kuna mwanafunzi mmoja alimaliza mitihani akaende sehemu ya starehe akawekewa madawa ya kulevya, wakambeba na kumbaka kisha akapata mimba, na miongoni mwa watu waliombaka alikuwepo mwathirika wa Ukimwi, Baba yake aliposikia akashituka sana na ikapelekea kifo chake” amesema Prof Mahonge.

Akizungumzia matumizi mabaya ya fedha Prof. Mahonge amesema kumekuwa na migogoro mingi ya matumizi ya fedha baina ya wanafunzi wenyewe na hata kwa mwanafunzi mwenyewe jambo linalosababisha kujikuta wameingia katika vishawishi vibaya.

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo Mwenyekiti wa Serikali ya Wanafunzi katika Kampasi ya Mizengo Pinda, Bw. Cosmas Milongo amesema elimu iliyotolewa na Kamati ya Kuthibiti Uadilifu itawasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.

“Vijana wanatakiwa kupewa elimu ya maadili kwani wamekuwa wakiongoza katika kuvunja maadili yakiwemo ya chuo na hata ya nchi,  kwa hiyo Kamati ina umuhimu mkubwa kwani inawasaidia wanafunzi kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingi kimaadili” amesema Milongo

Naye mwanafunzi katika Kampasi ya Mizengo Pinda Bi.Zainabu Omary amesema mafunzo hayo yamewajenga kwani katika dunia hii hakuna kitu kinaweza kwenda vizuri na kwa ufanisi kama maadili hayatazingatiwa.

Kwa upande wake Rebeka Ezekiel amesema wahanga wakubwa wa kukiukwa kwa maadili ni wenye jinsia ya kike kwani wakati mwingine wameingia katika vitendo visivyo na maadili kwa sababu ya shida walizonazo, lakini kupia mafunzo hayo wamejua namna sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo pasipo kukiuka maadili.

Pichani chini wanafunzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda wakishiriki mafunzo 👇





Post a Comment

0 Comments