SUAMEDIA

Serikali ya Tanzania yapongeza kurejeshwa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT)

 Na: Tatyana Celestine Manda

Waziri wa Kilimo nchini Mhe. Hussein Bashe awapongeza Wanachama na Wadau wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) kwa kukifufua chama hicho na  kurekebisha Katiba yao ili kuendana na mazingira ya sasa na ya baadae kwani kuwepo kwa chama kama hicho muhimu kinatoa nafasi kwa wanachama na wadau kubadilishana taarifa zao,  uzoefu kuhusiana na maendeleo ya kisayansi na kupeana mbinu za kukabiliana na changamoto katika kilimo.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussen Omary ameshiriki Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, katika Mkutano wa pili mwaka wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) jijini Dodoma

                 

Akifungua Mkutano wa pili mwaka wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) na kusoma Hotuba kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt. Hussen Omary amesema kuwa semina iliyofanyika imelenga maeneo muhimu na kipaumbele cha Wizara ya Kilimo ikiwemo kupeana taarifa na kujadili kuhusiana na mifumo ya mbegu, matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na maendeleo ya jumla ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Kilimo na mazao kwani vinachangia maendeleo ya nchi ya Tanzania kwa kuzingatia Hotuba ya kwanza ya Rais  wa  Samia Suluhu Hassan iliyolenga kuimarisha kilimo nchini.


Dkt. Omary ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kusimamia kilimo,  biashara, kuboresha mahusiano ya kimataifa ambayo yanaendelea kufungua fursa ya kibiashara , mifugo na uvuvi ndani na nje ya nchi hilo liijidhirisha  nchi ilipokuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) Afrika wageni kutoka nchi mbalimbali walishiriki na kufungua masoko zaidi ya mazao yanayozalishwa nchini


Aidha ameongeza kuwa malengo yanaweza kufikiwa endapo chama hicho kitakuwa na ushirikiano, mshikamano na usimamizi thabiti katika kutekeleza majukumu waliyojipangia kwani sayansi ya kilimo hutegemea ushirikiano wa wadau muhimu na wizara inaamini watatumia utajiri wa maarifa na ujuzi walionao wanachama wa CROSAT kutoka katika Taasisi za mafunzo ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) .


Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo pia ni mwanachama wa CROSAT kwa upande wa Tafiti Prof. Maulid Mwatawala amesema wao kama watafiti kuwa wanachama wa chama hicho itasaidia kuendelea kufanya tafiti ambazo zitawasaidia wakulima na watumiaji viuatilifu nchini kupata taarifa za utafiti wao kwa haraka ili kusaidia kupunguza athari zinazotokea kwa matumizi mabaya ya viuatilifu na kuepusha madhara kwa afya ya binadamu.


Prof. Mwatawala ameongeza kuwa watafiti hao wanafanya kazi kuhakikisha masoko ya kimataifa yanapatikana kulingana na masharti ya masoko ya kimataifa yanayohitaji bidhaa ambayo haijaathirika na wadudu hivyo wao watasaidia kuona namna ya kuhakikisha tafiti zinaleta matokeo chanya zitakazowezesha masoko kufunguliwa kimataifa.


Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu  Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndungulu amesema kuwa wao kama Mamlaka kuwa moja wa wanachama wa chama hicho wanapata fursa ya kusimamia matumizi sahihi ya viuatilifu , visumbufu vya mimea kama vile magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao na kufanya tija kuongezeka kwa kupanua usalama wa chakula na masoko nchini kuimarika.


Mkurugenzi huyo amesema kwa kupitia jukwaa hilo wanachama wanapata nafasi ya kupata taarifa za Mamlaka hiyo inavyofanya kazi ili kuleta maendeleo katika Sekta ya Kilimo na kuona mchango wa sekta hiyo katika nchi kutokana na mikakati ambayo mamlaka inaendelea kuitumia ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi salama ya viuatilifu  kama vile kutoa mafunzo kwa wazalishaji, wakulima na wafanyabiashara pamoja na kukagua viuatilifu vyote vinavyotumika nchini.


Aidha ametoa wito kwa wakulima, wafanyabiashara na wadau wanaojishughulisha na matumizi ya viuatilifu waweze kuwasiliana na mamlaka ili kupata miongozo ya mamlaka itawasaidia kufanya biashara zao kwa uhakika katika kufanya matumizi salama ya viuatilifu  kwani pamoja wataweza kulinda afya ya watanzania.


Mkutano wa pili mwaka wa Chama cha Taaluma ya Sayansi ya Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT)  wa siku mbili ulioanza 19/12/2023 na kuhitimishwa 20/12/2023  jijini Dodoma umeenda sambamba na uwasilishaji wa tafiti mbalimbali kutoka kwa wadau na wanachama wa chama hicho pamoja na kutoa majibu ya moja kwa moja yanayohusu changamoto mbalimbali za kilimo na matumizi ya viuatilifu Tanzania.















Post a Comment

0 Comments