SUAMEDIA

Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba awatunuku Wahitimu 3095 katika Mahafali ya 42 SUA

 Na, Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanya Mahafali yake ya 42 ambapo Wahitimu  3,095 kutoka programu 74 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu  elimu yao ya Chuo Kikuu ambapo  jumla ya watunukiwa wanawake ni 1,360 sawa na asilimia 43.9 ya Wahitimu wote na wanaume wakiwa 1,735 huku wakihudhurishwa kwa mara ya kwanza Wahitimu wa kwanza wa Ngazi ya Shahada kutoka Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi.

Amebainisha hayo Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda wakati akitaja takwimu za Wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Michezo vya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.

Katika takwimu hizo wahitimu 2,811 ni kutoka Shahada za Awali ambapo wanaume ni 1,574 na wanawake 1,237, Shahada za Umahiri wahitimu 56 wanaume 29, na wanawake 27, Stashahada ya Juu ya Elimu wahitimu 2 wote wakiwa ni wanaume, Shahada za Uzamivu 18, wanaume 10 na mwanamke 8, wahitimu wa Stashahada 140, wanaume 73 na wanawake  67 vilevile wahitimu 68 wa Astashahada , wanaume 47 na wanawake 21.

Aidha Prof. Chibunda amesema kuna vitu ambavyo Chuo kimeweza kutekeleza tangu kufanyika kwa sherehe ya Mahafali ya 41 ya Chuo chao yaliyofanyika Mei 25, 2023 ikiwemo shughuli za Mafunzo ambazo zimeendelea kufanyika kwa Kampasi zote tatu za Chuo hicho Edward Moringe, Solomon Mahlangu na Kampasi ya Mizengo Pinda Katavi vilevile katika mwaka wa masomo 2023/2024 Chuo kimesajili jumla ya wanafunzi wapya wa Shahada za Awali  5,254 na wanafunzi 195 wa masomo ya Uzamivu.

“Kwa sasa Chuo kina jumla ya wanafunzi 16,656 kati yao wanafunzi 15,476 ni wa Shahada za awali na wanafunzi 1,180 hawa ni wa Shahada za Juu,  aidha Miradi mipya ya Utafiti katika kipindi Cha mwezi Mei 2023 hadi sasa Chuo kimepata Miradi mipya 18 ua Utafiti yenye thamani ya shilingi bilioni 3.2”, alisema Prof. Chibunda

Prof. Chibunda amewashukuru wadau pamoja na washirika mbalimbali kwa misaada yao iliyochangia kukifikisha Chuo mahali kilipo huku shukrani zaidi akizipeleka kwa Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha Chuo chao kwa kulipia gharama muhimu za uendeshaji wa Chuo hicho  lakini pia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa msaada na Miongozo ambayo wamekuwa wakikipatia Chuo cha SUA na hivyo kukiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman amewakumbusha Wahitimu kuwa maisha Kitaaluma ni mitizamo ya maisha kwa ujumla yanayobadilika kila wakati  kutokana na misukumo mbalimbali ya Teknolojia na mazingira hivyo amewaomba Wahitimu hao kubadilika kulingana na mabadiliko hayo na kuyatumia kama fursa ili kuleta maendeleo.

Vilevile amewataka Wahitimu kutumia vyema fursa walizopewa na Serikali na ambazo zitajitokeza  kupitia programu mbalimbali katika kuwajengea uwezo na kuwawezesha kujiajiri kupitia Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili wakashiriki vyema katika shughuli za ujenzi wa nchi, hata hivyo amewapongeza kwa dhati wahitimu hao kwa mafanikio waliyofikia na kustahili kutunukiwa Tuzo walizofuzu.

“Kwa wale wanafunzi ambao hawajahitimu lakini wanazo ndoto za kuhitimu nawaasa kusoma kwa bidii ili watakapohitimu wawe na weredi wa kutosha katika fani zao kwasababu nisingependa  kuona wahitimu wa Chuo hiki chenye historia na uzoefu wa muda mrefu katika kufundisha masomo ya Fani za Kilimo wawe wasiojiamini katika kazi zao za kuhudumia watanzania”, alisema Jaji Mstaafu Mohamed Chande.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo  Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid  Mwatawala amesema Chuo kimeendesha program mbalimbali za masomo kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Kampasi zake zote tatu ikiwemo Astashahada 2, Stashahada 6, Shahada za awali 39, Stashahada za Uzamili 2, Shahada za Umahiri 57 na Shahada za Uzamivu.

KATIKA PICHA

 













PICHA NA NICHORUS ROMAN

Kwa video
fuata link -> https://youtu.be/lwSoxLSKlZg?si=f94AfmcQZfyzNewf

Post a Comment

0 Comments