Na Gerald Lwomile
Watumishi wa ngazi zote katika
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kufanyakazi kwa maslahi ya
Taasisi kwani maendeleo ya nchi na mahitaji yao kiuchumi yanategemea uwepo wa
Taasisi hiyo.
Prof. Christopher Mahonge akitoa mada katika semina (Picha zote na Gerald Lwomile) |
Akizungumza na watumishi wa Kampasi ya Mazumbai iliyopo mkoani Tanga Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU – SUA) Prof. Christopher Mahonge amesema ili nchi iwe na maendeleo inahitaji kuwa na watumishi wanaojituma katika kazi kwa kuzingatia uadilifu na kuepuka rushwa.
Amesema ni vyema watumishi
wakajua na kufahamu utawala bora ambao umebeba mambo mengi ikiwa ni pamoja na
uadilifu, uwajibikaji, uwazi, utawala wa sheria, haki bila upendeleo,
ushirikishwaji na kuepuka rushwa.
“Uwajibikaji hii ni nguzo muhimu
sana, sasa kuna vitu tunavipima kwa uwajibikaji yale majukumu ninayopewa je
ninayatekelezaje kufikisha malengo niliyopewa, kwa sababu kuna malengo ambayo
tumewekewa kila mtu kwa hiyo uwajibikaji ni muhimu sana” amesema Prof. Mahonge
Akizungumzia ushirikishwaji kazini Prof. Mahonge amesema pamoja na kuwepo viongozi ambao wana utaalamu katika maeneo yao ni muhimu wataalamu wanaohusika katika maeneo yao wakashirikishwa kumshauri kiongozi na si kiongozi kujiamulia tu kwani anaweza kufanya makosa kwa sababu hana utaalamu katika eneo jingine.
Kampasi ya Mazumbai |
“Na ili uwajibikaji uende vizuri
hapa tunajua kila mtu katika kitengo chake anatakiwa afanye nini, kuna
kuwajibika kwenda juu? mfano pale juu tuna Meneja wetu, kwa hiyo labda mtu
anasimamia kitengo fulani wale wafanyakazi wengine wanatoa taarifa kwa mwingine
kwa kufuata ngazi mpaka inamfikia Meneja” amesema Prof. Mahonge.
Akizungumzia mafunzo yaliyotolewa
na KKU-SUA Meneja wa Kampasi ya Mazumbai Bw. Steven Kingazi amesema semina
iliyofanywa na kamati hiyo ni muhimu kwa watumishi na ameiomba menejenti ya SUA
kuhakikisha kamati hiyo inaendelea kwenda katika Kampasi zake kutoa mafunzo
kwani mafunzo yatawakumbusha watumishi wajibu wao.
Meneja wa Kampasi ya Mazumbani Bw. Steven Kingazi akizungumza katika semina hiyo |
Amesema semina hiyo imetoa hamasa
na kuwakumbusha watumishi wajibu wa mtumishi wa umma katika kuhakikisha
watumishi wanaenenda katika misingi ya utawala bora.
“Hii inatusaidia kuhakikisha
sehemu ya kazi kunakuwa na uwazi, kunakuwa na uzingatiaji wa utawala wa sheria
na kanuni za utumishi wa umma, sehemu ya kazi inakuwa siyo sehemu ya kuomba au
kupokea rushwa lakini pia sehemu ya kazi inakuwa sehemu jumuishi, kila mtu kwa
kada yake na elimu yake anatakiwa kusikilizwa na kuhusishwa katika maamuzi”
amesema Kingazi.
Naye Afisa Misitu Bi. Agnes Ngao
na mfanyakazi katika Kampasi hiyo Bi. Zubeda Shemmela wamesema mafunzo hayo
yamewapa mwanga na uelewa wa mambo na wajibu wa mtumishi katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Habari picha ya matukio mbalimbali 👇
0 Comments