SUAMEDIA

Matumizi ya Akili Bandia kuboresha kilimo nchini.

 Na, Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Mkulima GPT chini ya ufadhili wa ‘BILL na MELINDA GATES Foundation’ imetoa mafunzo kwa wakulima wadogowadogo wapatao  20 mkoani Morogoro kuhusiana na Mfumo wa Akili Bandia unaotumia lugha ya kiswahili utakaomsaidia mkulima kuweza kupata ushauri kuhusiana na kilimo cha Mahindi kwa wakati husika lakini pia kutatua tatizo kwenye shamba lake bila uwepo wa Afisa Ugani.

Kiongozi wa Mradi huo na Mhadhiri Msaidizi SUA kutoka Idara ya Infomatikia na Teknolojia ya Habari Bi.Theofrida Maginga akizungumza na wakulima na wadau wa kilimo

Amebainisha hayo Kiongozi wa Mradi huo na Mhadhiri Msaidizi SUA kutoka Idara ya Infomatikia na Teknolojia ya Habari Bi.Theofrida Maginga wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye warsha iliyofanyika katika Hoteli ya Morena iliyoko Msamvu mjini Morogoro ambapo amesema Mkulima GPT ni ‘Chatbot’ inayowasaidia wakulima kupata taarifa ya namna ya kuandaa mashamba vilevile kusimamia mashamba ya kilimo cha mahindi kwa kutumia Akili Bandia ( Artificial intelligence).

Amesema lengo la kutumia Akili Bandia ni kwasababu ya ukuaji wa teknolojia hivyo wao kama watafiti kutoka SUA wanaangalia namna mbalimbali ambazo wanaweza wakatumia teknolojia kuwasaidia wakulima katika kufanya shughuli zao za kila siku japokuwa teknolojia inaweza kutumika si kwenye kilimo pekee bali hata kwenye maswala mbalimbali ya kijamii lakini kwa kuanza Mkulima GPT imelenga kuanza na kilimo cha Mahindi na hapo baadae wataangalia na mazao mengine,

Aidha Theofrida Maginga amesema wameleta Teknolojia hiyo kwa Wakulima ili wawe sehemu ya ukuaji wa teknolojia hiyo ndio maana wamefanya warsha ya kuwafindisha  Wakulima hao namna ya kutumia Mkulima GPT ili waweze kuanza kilimo cha kisasa ambacho kinafanyika si kwa kutumia Matrekta pekee lakini pia hata kutumia Akili bandia katika kufanya shughuli za kila siku kwa Mkoa wa Morogoro lakini pia na Tanzania kwa ujumla.

“Nafahamu kuwa sisi sote tunafahamu kuwa teknolojia ni changamoto kwa maeneo ambayo hayafikiki au maeneo ya vijijini sana lakini teknolojia inakuwa na lazima tujifunze kuwa nayo na lazima tutengeneze matokeo  ambayo yanaweza kuwasaidia wakulima kutumia hii hivyo basi mkulima anaweza akawa na namba ya simu ya ‘WhatsApp’ tu na akauliza swali kuhusiana na kilimo cha mahindi kwa kutuma ujumbe maandishi au sauti na moja kwa moja akapata majibu ya maelezo kutokana na swali alilouliza”, alisema Bi Theofrida Maginga

Akifungua mafunzo hayo Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Samwel Kabote amesema hatua uliyofikiwa katika matumizi ya Akili Bandia ni kubwa na itawasidia wakulima kupata taarifa kwa wakati.

Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Samwel Kabote akifungua mafunzo 

Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine kitaendelea kuhakikisha kinasaidia watafiti wachanga katika kuleta tafiti, ubunifu na teknolojia rafiki kwa wakulima ili ziwe na tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (SUA) Prof. Esron Karimuribo amesema teknolojia hiyo ni zaidi ya utafiti ni muendelezo wa kuboresha shughuli za Ugani kwa wakulima nchini ambapo Akili Bandia inatumika kusaidia katika kutoa ushauri wa papo kwa papo na kitu kizuri zaidi Utafiti huo umetumia lugha ya watanzania wengi ambayo ni kiswahili lakini pia imetumia ule mfumo wa ‘WhatsApp’ ambao watu wengi wameuzoea.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (SUA) Prof. Esron Karimuribo akizungumza katika mafunzo hayo

Amesema ili kuboresha matokeo makubwa ya kazi hii taasisi na vyombo husika na maswala yote ya Tehama pamoja na habari ikiwemo TCRA, EGA pamoja na Wizara ya Mawasiliano inabidi waione hii kama huduma muhimu kwa Taifa ikiwezekana yawekwe mazingira rafiki kuanzia bei za vifurushi na upatikanaji wa simu za ‘WhatsApp’ kwa njia rahisi ili wakulima wengi ambao wanahitaji huduma hiyo kuweza kuwa na nyenzo hizo pamoja na uwezo wa kidedha kuweza kupata huduma hiyo kwa haraka zaidi.

“Kupitia teknolojia hii kuna wakati hata hautahitaji Afisa Ugani katika eneo husika bali Afisa Ugani kiganjani  hivyo nitoe rai kwa wakulima kuanza mara moja kutumia teknolojia hiyo ambapo tupo sasa kwenye msimu wa kilimo hivyo natamani kuona mwaka huu huu teknolojia hiyo imeanza kutumika katika kuboresha mazao na tija ya uzalishaji hasa kwa zao la Mahindi”, alisema Prof. Esron Karimuribo

Naye Bi. Nia Sifanani ambaye ni Mkulima amesema kuwa mfumo wa Mkulima GPT ni mfumo mzuri ambao utaenda kuwasaidia wao kama wakulima kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili shambani na hata kwenye mazingira mengine hususani katika ufuatiliaji wa mazao hata hivyo ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kilimo nchini kuweza kuwasaidia katika upatikanaji wa mtandao kiurahisi hasa kwa wakulima waliopo vijijini.

Habari Picha 👇









Post a Comment

0 Comments