SUAMEDIA

Tafiti SUA zinaisadia Serikali uwekezaji kilimo- Katibu Tawala Iringa

Na Gerald Lwomile

Jitihada za Serikali katika kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo, kumepelekea Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta ya kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanga aliyekaa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliofikia katika kupata mrejesho wa utafiti, kulia waliokaa ni Prof. Karimuribo na kushoto ni Dkt. Helle Ravnborg (Picha na Gerald Lwomile)

Akizungumza mkoani Iringa katika siku ya kuwasilisha matokeo ya utafiti wa ‘Wawekezaji wa Kilimo ni wadau wa Maendeleo?’ (AIDA), Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanda amesema utafiti huo una manufaa makubwa kwa nchi ya Tanzania.

Amesema utafiti huo uliofanyika pamoja na kuwa na matokeo chanya katika baadhi ya maeneo, utaisadia Serikali kuboresha na kuhuisha Sera, Sheria na Miongozo yake iwe rafiki kwa wawekezaji na wadau wa kilimo ili kuakisi uhalisia kwenye mazingira ya nchi.

 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanga akifungua warsha ya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti

Akizungumza mara baada ya wasilisho la matokeo ya utafiti huu, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo amesema matokeo ya utafiti yameonyesha wazi mchango mkubwa na sera nzuri za uwekezaji za Tanzania.

Amesema kutokana na hali hiyo imepelekea wawekezaji kuwa na sehemu yao katika kutoa ajira japo si kwa kiwango kinachotarajiwa, pia rasilimali maji inapatikana katika maeneo wanayofanyia shughuli zao.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo akizungumza katika warsha hiyo

Awali akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mtafiti Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Evelyne Lazaro amesema pamoja na kuwa na lengo mahsusi katika utafiti huo lakini pia waliangalia uwekezaji na athari zake kwa maendeleo.

Amesema maeneo waliyoangalia katika eneo hilo ni athari katika upatikanaji wa ardhi, ajira na maendeleo kwa ujumla, pamoja na kuwa ajira imekuwa moja ya vigezo ili kuwepo kwa uwekezaji lakini matokeo yanaonyesha ajira ni chache ukilinganisha na matarajio.

“Kwa Tanzania haya mashamba makubwa hajaathiri sana mambo ya usalama wa ardhi na hii ni kwa sababu Tanzania tuna taratibu na sheria nzuri tu za mambo ya umiliki wa ardhi kwa wakekezaji na wananchi” amesema Dkt. Evelyne Lazaro.

Akizungumzia usalama wa chakula Dkt. Evelyne Lazaro amesema wawekezaji wamechangia kwa kiasi fulani kwani watu waopata kipato wana uwezo wa kununua chakula hivyo kuleta hali nzuri kwa kaya ambazo zinazunguka mashamba ya wawekezaji.

Dkt. Lazaro akitoa wasilisho la matokeo ya utafiti

Naye Prof. Khalmadin Mutabazi ambaye pia ni Mtafiti Mwandamzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema pamoja na kuwepo kwa nia njema ya uwekezaji lakini kulikuwa mazingira ya mkulima kunufaiaka na wakati mwingine kutonufaika na uwekezaji.

“Pamoja na kuja kwa fursa mpya kwa wakulima lakini nao wana mipango yao hivyo fursa inapokuja wanakuwa na wakati wa kipima na kuona nini kinaweza kuwasaidia zaidi mfano wakulima  wa Iringa na Njombe waliwekeza zaidi katika kilimo cha mbao lakini sasa wanawekeza zaidi katika kilimo cha parachichi” amesema Prof. Khalmadin Mutabazi.

Prof. Khalmadin Mutabazi akizungumza katika warsha hiyo

Naye Dkt. Helle Ravnborg kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kimataifa ya Dernmark (DIIS) amesema katika utafiti huo wameona kuna zaidi ya wawekezaji 100 katika sekta ya kilimo kutoka nchini Dermark ambapo wamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni wawekezaji binafsi, taasisi na makampuni ambapo wawekezaji binafsi ndiyo wanaonekana wana manufaa zaidi kwa jamii inayowazunguka tofauti na wale makampuni na taasisi.

Naye mkulima Nicodemus Malley, kutoka kutoka Kijiji cha Oldeani wilaya ya Karatu mkoani Manyara ameiomba Serikali kuhakikisha inawasaidia wakulima katika umiliki wa ardhi ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza baina yao na wawekezaji.

Amesema limekuwa jambo gumu kwa wakulima na wananchi wengine kumiliki ardhi lakini serikali inaweza kuwa na dhamira ya dhati ili kuweka usawa baina yao na wawekezaji ili kuhakikisha wanainua vipato vyao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto kupitia shughuli za kilimo.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo Mwafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) Festo Maro amesema katika utafiti huo imeonekana asilimia kumi (10%) ya wakulima wa maeneo Iringa na asilimia kumi na nane (18%) ya wakulima wa Njombe wamehamasika  kutoka kwa wawekezaji kulima mazao ya soya na parachichi ambayo awali hawakuwa wakiyalima.

Mwafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) Festo Maro akiwasilisha matokeo ya utafiti

Aidha matokeo hayo yameonyesha asilimia ishirini na sita (26%) ya wakulima wa Njombe walikuawanabadilishana taarifa na wawekezaji kuhusu mbegu mpya za mazao na teknolojia mpya za pembejeo na namna ya kupanda mazao huku Karatu ikiwa ni asilimia moja nukta mbili (1.2%) na Iringa asilimia kumi na sita (16%).

Katika matokeo mengine utafiti umeonyesha asilimia sabini na nne (74%) ya wakulima wadogo mkoani Iringa walipata pembejeo na kemikali kutoka kwa mwekezaji huku Njombe ikiwa ni asilimia ishirini na sita (26%), matokeo hayo pia yameonyesha kuwa asilimia sitini na mbili (62%) ya wakulima kutoka Njombe waliingia makubaliano na wawekezaji kulima mazao kwa kuzingatia kiwango cha ubora katika uzalishaji wa mazao.

Utafiti huu unaoitwa ‘Wawekezaji wa Kilimo ni wadau wa Maendeleo?’ (AIDA) umetekelezwa na SUA, Chuo Kikuu cha Makerere, Denmark na Taasisi ya mafunzo ya Kimataifa cha Dermark ukishirikishwa wadau mbalimbali katika maeneo ya Karatu, Iringa na Njombe na kufadhiliwa na Shirika na Maendeleo la Dernmark (DANIDA).

Chini ni picha zikionyesha matukio mbalimbali katika warsha hiyo 👇


















Post a Comment

0 Comments