SUAMEDIA

Afrika inahitaji na ipo tayari kwa teknolojia mpya za kilimo ili kuzalisha

 Na: Calvin Gwabara – Nairobi.

Rais wa zamani wa Nigeria Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan amesema mawasilisho na majadiliano ya wadau kwenye mkutano wa Teknolojia za Kilimo Barani Afrika yamedhihilisha kuwa bara la Afrika linahitaji teknolojia ilikuweza kulisha ongezeko kubwa la idadi ya watu waliopo na kujiandaa na wanaokuja.

Rais wa mstaafu wa Nigeria Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan akitoa hotuba ya ufungaji wa mkutano wa ACAT.

Ameyasema hayo wakati akifunga mkutano wa kwanza wa Teknolojia za Kilimo Barani Afrika uliofanyika nchini Kenya na kuwakutanisha mamia ya wadau wa kilimo kutoka Afrika yote na Duniani ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya kupitia Wizara yake ya Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji na Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika AATF.

“ Nitumie nafasi kuwaomba kuiendeleza ACAT kama sehemu muhimu ya kuonesha Bunifu Sayansi na  Teknolojia za Kilimo wakati tukiendelea kwenye kupambana kutengeneza mazingira wezeshi kwa ukuaji wake na hivyo niwaombe wawekezaji zaidi hasa wanaofanyakazi Afrika kwenye Teknolojia za Kilimo Afrika kuunga mkono jitihada hizi za ACAT,” alisema Mhe. Dkt. Jonathan.

Aidha amesema mkutano wa ACAT umeonesha kuwa mazingira ya kilimo Afrika yapo tayari kwaajili ya mabadiliko na mbegu ya ubunifu ipo tayari kupandwa hivyo lazima kutumia rasilimali zilizopo na kufanya uwekezaji mzuri ili kupata Ubunifu unaohitajika kwa kilimo chenye mafanikio Afrika.

Rais huyo wa zamani wa Nigeria amesema bado kuna matumaini na zipo fursa za kufungua sura mpya katika juhudi za kuboresha kilimo, ugani na ustawi wa watu lakini  hii haiwezekani kufanyika kwa kuachiwa Serikali pekee.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF) Dkt. Canisius Kanangire amesema ukuaji wa vijana barani Afrika unaweza kuleta mabadiliko katika sekta hiyo huku zaidi ya 80% ya wabunifu wakiwa vijana na hivyo Serikali na wadau wamepewa changamoto kutazama upya nafasi ya vijana.


Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF) Dkt. Canisius akitoa maazimio ya mwisho ya mkutano huo kwa niaba ya washiriki wote.

“Umuhimu wa kuweka mazingira wezeshi na vivutio vya kutosha kuwezesha Utafiti, maendeleo na ubiasharishaji wa Teknolojia za Kilimo biashara ya ubunifu wa kilimo na uanzishwaji wa sekta binafsi inayofanya kazi unahitaji kusisitiza kwa kasi” alisisitiza Mkurugenzi huyo wa AATF Dkt. Kanangire.

Aidha Dkt. Kanangire ametoa wito wa kuwajengea uwezo wakulima uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabia nchi barani Afrika, ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa Kilimo na mifumo ya chakula barani humo huathirika sana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo wa siku tano umefanyika nchini Kenya na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali za afrika na nje ya Afrika.

       



Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya AATF Prof. Aggrey Ambali akitoa salamu za Bodi wakati wa ufungaji wa mkutano huo wa wa siku tano ACAT jijini Nairibi.


Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya AATF Prof. Aggrey Ambali pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF) Dkt. Canisius Kanangire wakimkabidhi tuzo ya heshima Rais wa zamani wa Nigeria Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan ambaye pia ni Balozi wa AATF kwa mchango wake katika kusaidia wakulima barani afrika kupata teknolojia.

 
















Post a Comment

0 Comments