SUAMEDIA

Tanzania inavyosaidia Wakulima na Wafugaji kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

 Na: Calvin Gwabara – Nairobi.

Tanzania kupitia Wizara yake ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikitekeleza mbinu mbalimbali za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa Wakulima na Wafugaji nchini.

Bw. Kamwesige Mujuni Mtembei ambaye ni Afisa mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo nchini Tanzania wakati akizungumza kwenye  Mkutano wa ACAT.

Hayo yameelezwa na Bw. Kamwesige Mujuni Mtembei ambaye ni Afisa mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo nchini Tanzania wakati akizungumza kwenye mjadala uliohusu juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kusaidia jamii kukabiliana na athari hizo kwenye mkutano wa teknolojia za kilimo barani Afrika unaoendelea Jijini Nairobi nchini Kenya na kukutanisha mamia ya wadau wa kilimo Afrika na  Duniani.

“Tanzania ni kati ya nchi zilizoathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi kama vile ukame,mafuriko katika baadhi ya maeneo na kupanda kwa viwango vya joto, hivyo Wizara kupitia mikakati na miongozo ya kilimo himilivu inawaelimisha wakulima namna ya kuboresha kilimo na ufugaji ili kuongeza tija” alieleza Bw. Mtembei.

Aliongeza “ Kwa kutambua kuwa Vijana na wakina Mama ni waathirika zaidi wa tatizo hili Serikali inaendesha program ya Jenga Kesho Bora (BBT) ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa mashamba yenye miundombinu ya umwagiliaji na upatikanaji wa mitaji na masoko kwa wakina Mama na vijana”.

Amesema kuwa Wizara inaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuhamasisha Utafiti na uzalishaji wa mbegu bora sambamba na kuongeza bajeti ya utafiti wa mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo himilivu cha mabadiliko ya tabia nchi.

Afisa huyo mwandamizi wa kilimo amesema Wizara inaendesha miradi  ya kutoa pembejeo za ruzuku ili kuwezesha wakulima kumudu matumzi ya pembejeo katika kuongeza tija.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya kupitia Wizara yake ya Kilimo na maendeleo ya Ufugaji na Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika AATF na unawakutanisha wadau wa kilimo kutoka afrika na pande zote za Dunia.


PICHA ZA WADAU WAKATI WA MJADALA HUO


Mchokoza mada wa mjadala huo ambaye ni Makamu Mkurugenzi wa misheni wa USAID nchini Kenya Bi.Sheila Roquitte   akichokoza mada.

Picha ya Pamoja ya wachangia mada wazungumzaji wa mjadala huo








Post a Comment

0 Comments