Na Gerald Lwomile
Wizara ya Kilimo nchini imesema itaendelea kuwa na ushirikiano
na Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) katika kuhakikisha inainua
sekta ya kilimo nchini ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya wakulima.
Mratibu Wizara ya Kilimo Mashirikiano ya Kimataifa Bibi. Daines Mtei aliyevaa kilemba katikati akipata maelezo mbalimbali kutoka kwa wadau wa kilimo |
Akizungumza katika sherehe za mwaka mmoja tangu kuanza kwa Program
ya Kilimo Tija inayoendeshwa kwa ufadhili wa USAID, Mratibu Wizara ya Kilimo
Mashirikiano ya Kimataifa Bibi. Daines Mtei amesema Wizara imekuwa ikitaka
kuhakikisha kilimo kinamnufaisha mkulima, kiwe cha ajira na kitengeneza kipato
kwa mkulima ili aweze kuendesha maisha yake.
Bibi. Mtei amesema nchi imepata matokeo chanya katika kilimo
kupitia misaada mbalimbali inayotolewa na USAID na kuongeza uzalishaji wa mazao
ya kilimo hivyo wanaona umuhimu wa kuwepo kwa shirika hilo la misaada nchini.
Amesema ushahidi wa matokeo hayo chanya unathibitishwa na
ushirikiano ulipo baina ya Chuo cha Kilimo MATI Ilonga na USAID kupitia mradi
huo wa Kilimo Tija ambapo malengo kadhaa yamefikiwa ikiwa ni pamoja na
kuboresha mifumo ya masoko ya mbogamboga na matunda ili kupanua wigo wa fursa
za ajira na uchumi.
Amesema katika kutekeleza ushirikiano huo USAID imewezesha
uwepo wa miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo bwawa, pampu na mazao ya kuanzia
huku chuo cha MATI Ilonga kikijikita katika kuunganisha miundombinu hiyo pamoja
na eneo la kutekeleza mradi huo.
Mratibu Wizara ya Kilimo Mashirikiano ya Kimataifa Bibi. Daines Mtei akizungumza katika sherehe za mwaka mmoja wa Kilimo Tija |
Awali akizungumza katika sherehe hizo Mkuu wa Program ya
Kilimo Tija Tanzania Bw. Antonia Coello amesema katika utekelezaji wa program
hiyo ndani ya mwaka mmoja kuna mafanikio kadhaa ambayo wamepata ikiwa ni pamoja na zaidi ya
asilimi 56 ya wadau waliotegemea kushiriki katika program miongoni mwao elfu
saba ni vijana na asilimia 39 ni wanawake.
Mkuu wa Program ya Kilimo Tija Tanzania Bw. Antonia Coello akizungumza wakati wa sherehe hizo |
Amesema program hiyo hadi sasa imewafikia wakulima wadogo na
wa kati 277 huku zaidi ya shilingi bilioni 3.9 zikitumika katika kutekeleza
program hiyo ya Kilimo Tija ambapo mambo kadhaa yamefanyika ikiwa ni pamoja na
kutoa mitaji, vifaa na teknolojia
mbalimbali ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Naye Naibu Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Ukuzaji Uchumi ya
Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani USAID Bw. Plato Hieronimus amesema utekelezaji
wa program hiyo katika Chuo cha Kilimo MATI Ilongo ni moja kati ya majukumu yao
waliyojiwekea ili kusaidia maendeleo katika nchi ya Tanzania.
Amesema ili wakulima wajue mbinu bora za kilimo ikiwa ni pamoja
na kilimo cha umwagiliaji ni muhimu wakapata mafunzo na kujua namna bora zaidi
ya kufanya kilimo na hilo litaletwa na uhusiano imara zaidi kati ya Wizara ya
Kilimo, Wadau na Sekta binafsi kwani bila wao ni vigumu kuwa na muendelezo
katika kilimo.
Naibu Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Ukuzaji Uchumi ya Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani USAID Bw. Plato Hieronimus akipanda mche wa nyanya |
Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa sherehe hizo Mkuu wa Chuo cha Kilimo Ilonga Bw. Felix Mrisho amesema Chuo hicho kimeingia makubalianao na Mradi wa Kilimo Tija ambao ulianza tarehe 14 Aprili, 2023 lengo likiwa ni kutoa mafunzo kwa vijana.
Amesema wamefundisha vijana wengi wakiwemo wale wa BBT Pamoja
na vijana wanaosoma katika chuo hicho cha MATI Ilonga na wamefundishwa mambo
mbalimbali ikiwa ni Pamoja na kuchagua eneo sahihi la uzalishaji, namna ya
kuandaa shamba, matumizi ya mbolea, kufunga mifumo ya umwagiliaji na matumizi
bora ya maji na namna ya kupambana ili mazao yasishambuliwe na wadudu na kilimo
biashara.
Mkuu wa Program ya Kilimo Tija Tanzania Bw. Antonia Coello (wa pili kulia) akibadilishana mkataba wa makubaliano na Mkuu wa Chuo MATI Ilonga Bw. Felix Mrisho akiyevaa kofia wakati wa sherehe hizo |
0 Comments