Na: Winfrida Mwakarobo
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia kituo chake cha habari cha SUA Media kimeanza kufanya uhamasishaji kwa watu kufuatilia matangazo yake ya redio na mitandao yake ya kijamii ili kujua na kupata elimu juu ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, hifadhi ya mazingira na afya.
Mkazi wa mtaa wa Konga Kata ya Kauzeni aliyeshika kipaza sauti (katikati) akitoa maoni yake wakati wa mkutano wa uhamasishaji |
Akizungumza na wananchi wa mtaa wa Konga, Kata ya Mzinga Manispaa ya Morogoro Oktoba 9, 2023 Bw. Gerald Lwomile ambaye ni Msimamizi wa Kituo cha habari cha SUA Media amesema kuwa lengo la ziara hiyo ya uhamasishaji ni kuijulisha jamii umuhimu wa kufuatilia vipindi mbalimbali vinavyorushwa na redio ya SUA FM 101.1 ikiwa ni pamoja na kipindi kipya cha Sauti ya Tiba.
“Kwa
miaka mingi tumekuwa tukiona hali si njema sana kwa wakulima walio wengi hivyo
kuonekana kama kilimo hakilipi lakini ukweli ni kuwa kilimo kinalipa endapo tu
kitafanyika kitaalam kwa kutumia mbinu
bora za kilimo zinazoambatana na teknolojia za kisasa kuanzia upimaji wa
udongo, uandaaji wa shamba, upandaji na uvunaji, na kwa kweli SUA imekuwa
ikitoa ushauri kwa wakulima” amesema
Lwomile
Msimamizi wa Kituo cha SUA Media Gerald Lwomile akiongea na wananchi wa mtaa wa Konga Kata ya Kauzeni |
Bw.
Lwomile amesema kupitia redio hiyo msikilizaji anaweza kusikia ushauri
mbalimbali unaotolewa na watafiti waliobobea katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kilimo, ufugaji, uvuvi, hifadhi ya mazingira, misitu, wanyapori na afya ujumla.
Amesema
SUA FM hivi sasa mbali na kurusha vipindi hivyo lakini imeanzisha kipindi kipya
kwa kushirikiana na Taasisi inayofanya utafiti wa Kiuchumi na Jamii ‘Economic and Social
Research Foundation’ na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
kipindi kinachowapa fursa watu kujua afya zao na namna ya kujikinga na kupata matibabu
sahihi.
Amesema kupitia
kipindi hicho SUA FM itakuwa ikiwalika wataalam mbalimbali wa afya na wananchi
ili kujadili na kujua afya zao, kipindi hicho hurushwa hewani kupitia masafa ya
FM 101.1 kila siku ya Jumamosi saa 3 asubuhi na kurudiwa Jumatano saa 5 asubuhi.
Kwa upande
wake Diwani wa Kata ya Mzinga Manispaa ya Morogoro Mhe. Salum Mrisho Chunga amesema
kuwa wanaishukuru SUA FM kwa kuwakumbuka na kuwatembelea ili kuwaelewesha na kuwaelimisha wananchi nini
SUA inafanya lengo likiwa kuwasaidia wakulima kulima kwa tija na kuwaondoa
kwenye umasikini hivyo ziara hiyo imekuwa chachu kubwa kwa Kata yao na kuahidi
kutengeneza mahusiano ya karibu na mazuri na wataalam kutoka SUA ili waweze
kupata elimu ya kutosha kuhusiana na Kilimo.
Diwani wa Kata ya Mzinga Manispaa ya Morogoro Mhe. Salum Mrisho Chunga akizungumza na wana mtaa wa Konga |
Naye Nassoro Ramadhani Mkazi wa Mtaa wa Konga B kata ya Mzinga amesema wamekuwa wakikubwa na usumbufu wa ugonjwa wa mnyauko wa mazao ikiwemo migomba, mbogamboga na mazao mengine hivyo wanatumaini kupitia ziara SUA Media basi watafikisha taarifa hiyo kwa watafiti wa SUA ili wapate ufumbuzi wa matatizo hayo ambapo Bw. Lwomile ameahidi kufikisha changamoto hiyo kwa uongozi na watafiti SUA.
0 Comments