SUAMEDIA

AATF kuwakutanisha wadau wa Teknolojia za Kilimo Africa.

 Na: Calvin Gwabara.

Serikali ya Kenya kupitia Wizara yake ya Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika wanatarajia kuwakutanisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo kwenye uzinduzi wa mkuatano wa kwanza wa Teknolojia za kilimo Afrika.

Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji ya Kenya Bwana Phillip Harsama (Kkushoto) na Dkt. Canisius Kanangire ambaye ni  Mkurugenzi Mtendaji wa AATF  (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa ACAT.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na maendeleo ya Ufugaji ya Kenya Bwana Phillip Harsama, wakati akizungumza kuhusu maandalizi na malengo ya mkutano huo mkubwa na wa aina yake Barani Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 30/10/2013 hadi tarehe 03/11/2023 Jijini Nairobi nchini Kenya na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kwanza kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa ACAT.

” Kama nchi tunayo furaha kuwa mwenyeji mwenza kwenye uzinduzi wa ACAT 2023 na tunaukaribisha ulimwengu,Kanda na jumuiya za ndani kwenye jukwaa hili muhimu na tunatarajia kujadili suluhu zinazotekelezeka katika kitatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ambazo pia zitasukuma mabadiliko yatakayopeleka ukuaji wake” alisema Bwana Harsame.

Aliongeza “Mkutano huu umekuja wakati muafaka ambapo Bara la afrika linahangaika kulisha watu wake huku mabadiliko ya tabia nchi yanaleta changamoto kubwa kwa ustawi wa watu kwa ujumla”.

Ameongeza kuwa Mkutano huo wa ACAT utatumika kama jukwaa kuu la kuendeleza uhamasishaji wa teknolojia za kilimo barani afrika na kutetea matumizi ya ubunifu lakini pia mkutano huo wa mwaka huu utaangazia bunifu mbalimbali zinazoibukia ndani ya sekta ya teknolojia za kilimo.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji ya Kenya amesema Mkutano huo utawaleta pamoja wawakilishi wa Serikali, Viwanda kupitia Viongozi wao,Watunga Sera, Wataalamu wa kiufundi, Taasisi binafsi,Wakulima,Wanawake na Vijana ulimwenguni kote kujadili na kufafanua hatua za kiutendaji na masuluhisho ya changamoto za upatikanaji na matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake Rais wa zamani wa Shirikisho la Jamhuri la Nigeria ambaye pia ni Balozi wa AATF Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan ameeleza kuunga mkono mkutano huo akibainisha kuwa kilimo kina jukumu muhimu katika Ajenda ya kiuchumi ya afrika na kinamchango mkubwa katika ajira,Usalama wa Chakula na ukuaji wa uchumi.

Rais wa zamani wa Shirikisho la Jamhuri la Nigeria ambaye pia ni Balozi wa AATF Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan.

“ACAT utatoa fursa kwa wadau kuzungumza na kusonga mbali zaidi ya majadiliano  kuhusu teknolojia mpya ili kuzishikilia na kisha kuzitumia ” Alisema Rais huyo wa zamani.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa AATF Dkt. Canisius Kanangire amesema ACAT utaangazia matumizi ya Sayansi teknolojia na Ubunifu katika kukuza mageuzi ya kilimo hasa katika kushughulikia changamato kuu zinazowakabili wakulima wa kiafrika.

“Mara nyingi nafasi ya Sayansi teknolojia na Ubunifu kwenye sekta ya Kilimo hayajazingatiwa hivyo ACAT ni fursa ya kuonesha kikamilifu na kusherehekea mchango wa STI katika kuimarisha usalama wa chakula na maisha ili kuhimiza mazungumzo na ubunifu” Alieleza Dkt. Kanangire.

Dkt. Canisius Kanangire ambaye ni  Mkurugenzi Mtendaji wa AATF  (Picha na Kilimo news)

Aliongeza “Mkutano huo utaongeza juhudi za kuanzisha ushirikiano na mashirika yenye nia moja yanayofanya kazi katika sekta ya teknolojia ya kilimo na kutoa fursa kwa wadau kupeana taarifa kuhusu teknolojia mpya za kilimo zinazoibukia.

Aidha amesema kuwa AATF imekuwa mstari wa mbele kuwezesha upatikanaji, maendeleo na ubiasharishaji wa teknolojia za kilimo hivyo mkutano huu utasaidia kuzitazama ubunifu zinazoweka kuleta mabadiliko makubwa na kuangazia fursa za kushughulikia matatizo mengi yanayoikabili sekta hii kutokana na idadi ya ongeeko la watu, Mabadiliko ya hali ya hewa na mambo mengine.

Hata hivyo Dkt. Kanangire pia amesema ACAT inatoa jukwaa adimu la kujadili vikwazo vya uhauwilishaji wa teknolojia na kushauri mikakati ya kufanya mageuzi teknolojia zilizopo kwenda kwenye teknolojia za kisasa ambazo zinauwezo wa kuongeza uzalishaji na kushughulikia changamoto zinazowakabili wakulima wa afrika.

AATF imejidhatiti katika kukuza uhamasishaji wa teknolojia za kilimo ambazo zinashughulikia vikwazo vya uzalishaji wa wakulima kwa kufanyakazi na wadau kutoka bara zima Kwa teknolojia 24 zilizo kwenye nchi 24 zenye thamani ya shilingi dolla za kimarekani milioni 650 na kufikia wakulima wadogo milioni 4.8 kwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Post a Comment

0 Comments