Na: Calvin Gwabara – Nairobi.
Waziri wa Elimu Sayansi na
Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameongoza timu ya Serikali ya Tanzania kwenye
mkutano mkubwa wa Teknolojia za Kilimo Afrika (ACAT) ulioanza leo jumatatu
nchini Kenya.
Mara baada ya kufika kwenye
viwanja vya mkutano huo mkubwa akiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya
Mhe. Balozi Dkt. Benard Yohana Kibesse pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya
Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu na watumishi wengine wa
Serikali ametembelea maonesho mbalimbali ya Teknolojia za kilimo zinazooneshwa
nje ya mkutano huo.
“Nimeona maonesho ambayo kimsingi
ni kuhusu jinsi Sayansi na Teknolojia inavyoweza kuleta mabadiliko chanya
kwenye kilimo pamoja na ukweli huu tumeona pia umuhimu wa kuzingatia usalama na
afya kwenye mabadiliko haya na pia kuchukua tahadhari tusipoteze umiliki wa
yale tunayogundua, hasa mbegu bora, ili tusiingie kwenye utegemezi utakaotudhoofisha”
alisema Prof. Mkenda.
Tanzania kupitia wizara yake ya
Elimu Sayansi na Teknolojia na taasisi zilizo chini yake imekuwa ikitoa mchango
mkubwa katika kuhakikisha nchi inawezesha wabunifu kupitia Programu zake
mbalimbali ikimwemo Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (
MAKISATU) ambayo yanafanyika kila mwaka kwa kuhusisha wabunifu mbalimbali
kuanzia kwenye jamii, Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo Vya kati, Vikuu pamoja
na Taasisi za Utafiti na kuwapatia washindi fedha na mahitaji mengine ili
kuwezesha kukuza bunifu zao na kuzibiasharisha.
Aidha Mkutano huo wa (ACAT)
umeandaliwa na Serikali ya Kenya kupitia Wizara yake ya Kilimo na Maendeleo ya
Ufugaji kwa kushirikiana na Taasisi ya Teknolojia za Kilimo Afrika (AATF).
0 Comments