Na:Asifiwe Mbembela
Waboreshaji
na Wakuza Mitaala wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa
HEET wamehimizwa kuendelea na mchakato wa kuandaa mitaala mipya ya kidigitali ili
kuendana na mpango ya Chuo unaoitaka mitaala hiyo kupelekwa kwa wadau wake
ifikapo Oktoba 11 mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Uboreshaji na Ukuzaji wa Mitaala SUA Dkt. Jamal Jumanne Athuman wakati akihitimisha mfululizo wa semina za mafunzo kwa wakuza mitaala wa Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo Mjini Mpanda mkoani Katavi.
Dkt.
Jamal amebainisha kuwa mitaala ambayo inaendelea kuboreshwa na kukuzwa na Wahadhiri
wa Kampasi zote tatu (Edward Moringe, Mizengo na Solomon Mahlangu) inatakiwa ikamilike
kabla ya Oktoba 10 ili kuruhusu tarehe inayofuata kupelekwa kwa wadau kwa ajili
ya mapitio ya awali ya mitaala hiyo.
‘‘Leo tumehitimisha mafunzo hapa Kampasi ya
Mizengo Pinda ambapo tulikuwa na wawezeshaji wanne kila mmoja akiwasilisha
kwenye eneo lake, sasa tunaanza zoezi lenyewe ambapo wakuza mitaala wanatakiwa
kuhakikisha mpaka tarehe 11 ya mwezi wa 10 hii mitaala iwe tayari kwa ajili ya
kupelekwa kwa wadau ili ijadiliwe zaidi”, alisema Dkt. Jamal ambaye pia ni
Amidi wa Shule Kuu ya Elimu, SUA.
Amesisitiza
kuwa mitaala ambayo inaenda kuboreshwa itakuwa ni mitaala ujuzi ambayo
inajikita katika kumuandaa mhitimu mwenye uwezo mkubwa kinadharia pamoja na
vitendo.
Dkt.
Prisila Mkenda mmoja wa wawezeshaji wa mchakato wa uboreshaji na ukuzaji
mitaala hapa chuoni akijikita katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi
amesema kupitia maboresho hayo, wakuza mitaala wanatakiwa wajumuishe masuala ya
hali ya hewa ili kutoa nafasi ya jamii kujifunza na kupata uelewa kuhusu
mabadiliko ya tabianchi na namna gani ya
kudhibiti athari zaidi kwa kuanzia na wanafunzi.
Amesema
wanaona kama kwenye mitaala mipya kutakuwa na vipengele ambavyo vitaelezea
mabadiliko ya tabianchi, wanafunzi watakuwa na uelewa wa kukabiliana na hali
hiyo ikiwemo majanga ya mafuriko, ukame, pia kujua namna ya kukabiliana na
wadudu waharibifu ambao wanachagizwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mwezeshaji
Prof. Ernest Kira ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi SUA akizungumzia kuhusu
uandaaji wa mitaala mipya ya kidigitali amesema kwenye mitaala inayokuja
wanakusudia kujumuisha umahiri wa
kutenda kwa nadharia na vitendo ili wahitimu waendane na mahitaji ya soko.
Kwa
upande wake, Dkt. Alcardo Barakabitze ambaye ni Mhadhiri wa SUA na mwezeshaji
amewaambia washiriki wa mafunzo hayo Kampasi ya Mizengo kuwa, Chuo kinaendelea
kujipanga na mabadiliko ya mitaala kwani kinakusudia kuongeza ufanisi na
upatikanaji wa intaneti ili wanafunzi na waalimu waweze kuimudu mitaala mipya
ya kidigitali.
Evaristus
Aloyce, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akiongea baada ya mafunzo amesema
maboresho ya mitaala ambayo wamepewa ujuzi ni muhimu kwani yataboresha maeneo ambayo walikuwa wanayafanyia kazi katika mitaala ya nyuma.
0 Comments