SUAMEDIA

SUA ina mchango mkubwa kukuza Uchumi wa Buluu

 Adam Maruma

Imeelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, (SUA) kupitia kwa wataalam wake wabobezi  wa Elimu ya Viumbe maji,  ina mchango mkubwa katika kufanikisha ndoto ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini Rais Dk. Hussein Mwinyi kuwainuia wanachi wa visiwa hivyo kiuchumi kupitia matumizi ya rasimali zilizopo baharini maarufu kama Uchumi wa Buluu.

Mkutubi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo Bi. Editha Njau akijibu swali lililoulizwa na mmoja wa waalimu wa shule ya Sekondari Ben Bela

Hayo yamesemwa na Mwalimu Nahida Yusufu Septemba 29, 2023 wakati akitoa neno la shukrani walipofanya ziara ya siku moja chuoni hapo ambapo wanafunzi pamoja na walimu wao kutoka shule ya Sekondari  ya Wasichana ya Ben Bela iliyopo Unguja Zanzibar, wamefanya ziara ya siku ya mafunzo ya siku moja SUA na  kujifunza kupitia wataalam wa idara za  chuo hicho wakiwemo wataala wa shamba la viumbe maji na  mifugo wengine wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Mwalimu huyo ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa na shauku kubwa ya kuwakwamua wananchi kiuchumi kupitia rasilimali za bahari na hivyo kwa kupitia elimu waliyopata SUA, haswa ufugaji wa Samaki kisasa wameona chuo hicho kinatoa elimu ambayo kwa kiasi kikubwa wananchi na hasa wanafunzi wa Zanzibar wanatakiwa kuipata ili kuweza kuelewa namna ya kufaidika na uchumi wa Buluu.

‘’Kwa mfano kwa sasa sisi Unguja tuna hili suala la Uchumi wa Buluu, kwa vile tunazo rasimali nyingi za bahari sasa moja kwa moja kama elimu hii haswa ya mabwawa ya kisasa ambayo tumeelezwa na wataalam hawa wa SUA tunaweza kufika mbali zaidi kama tutaitumia elimu hii kule kwetu Unguja na hivyo tutakuwa tumeziunga mkono Serikali zetu zote mbili katika juhudi za kuwakwamua wananchi kiuchumi’’ amesema Mwl. Nahida Yusufu.

Mwanafunzi Rehema Ali Bushiri akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwao kwa kuwa wamekuwa akiisikia SUA kwa muda mrefu kama Chuo Kikuu cha Kilimo kikongwe  nchini lakini sasa wamefahamu chuo kilivyo na wamehamasika  kuja kusoma chuoni hapo katika siku zijazo baada ya kuhitimu masomo yao na kufaulu vizuri na hatimae kujiunga SUA  kwa masomo ya  elimu ya juu.

‘’Tumekuwa tukiisikia SUA kwa muda mrefu kama Chuo kikongwe kwenye Kilimo na hatimae leo tunafurahi kuwa hapo na hii itatufanya tuongeze bidii katika masomo yetu ili siku moja na sisi tuwe wanafunzi wa chuo hiki kwa masomo ya elimu ya juu na kuweza kuipeleka taaluma hii Zanzibar ili wananchi waweze kufaidika na elimu na haswa elimu ya viumbe wa maji ni muhimu sana kwa wananchi wa Zanzibar’’ amesema Rehema Bushiri.

Wanafunzi hao wapatao 57 wameambatana na walimu wao 7 wameishukuru SUA kwa kuweza kuwakubalia kufika chuoni hapo na kuweza kufahamu mambo ambayo walikuwa hawana ufahamu nayo na kusifu  mapokezi mazuri kutoka idara ya Mawasiliano na Masoko ya SUA tangu kufika na hadi kuondoka chuoni hapo na kuahidi ziara hiyo itakua endelevu katika siku zijazo

Shule ya Sekondari ya wasichana Ben Bela ni miongoni mwa shule kongwe zaidi iliyopo Unguja, visiwani Zanzibar na ifikapo mwaka 2024 shule hiyo itakuwa inaadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake 1924.

Mtaalam wa Viumbe Maji Bw, Alfred Thomas akitoa maelezo ya namna ya kutotolesha vifaranga vya samaki








Post a Comment

0 Comments