Na, Winfrida Nicolau
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimezindua Dawati la Jinsia chuoni hapo ili kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii hususani chuoni hapo.
Dawati hilo limezinduliwa leo Octoba 10, 2023 na Prof. Samweli Kabote Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda ambapo amesema atafurahi kuona Dawati hilo likiwa chachu ya kuimarisha maendeleo ya Jinsia katika maeneo chuo na yanayozunguka chuo hapo.
Amesema kumekuwa na kuna mambo mengi yanayofanyika katika maeneo hayo na hawayasikii lakini yapo na yanaendelea hivyo amelitaka Dawati hilo kufanya utafiti na kuyaibua mambo ili kuimarisha swala zima la maendeleo ya Jinsia kama sehemu ya Taaluma inayopaswa kuchapishwa katika machapisho ya aina mbalimbali
"kwa vile tunao Wataalamu waliofunzwa vizuri kwa namna ya kufanya Tafiti watusaidie, wapo wataalam wa Sosholojia lakini wapo wataalam wa masuala ya Jinsia hapa chuoni kwaiyo watusaidie kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuyaibua yale matatizo ambayo yapo na atuyasikii kwa kushirikiana na kamati yetu pia kwaajili ya kuyafanyia kazi " amesema Prof. Kabote.
Kwa upande wake Prof. Geoffrey Karugila Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi akimuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Utawala na Fedha SUA Prof. Amandus Muhairwa amesema wanatambua kuwa kila mtu bila kujali jinsia yake anauwezo na mchango wa pekee katika maendeleo ya Taasisi yao hivyo wanakusudia kujenga mazingira ambayo yatawezesha wanajumuiya wote wa SUA kufikia uwezo wao kamili wa kiutendaji bila kujali jinsia zao.
"Zoezi hili linahitaji jitihada zetu za pamoja katika kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa za elimu, ufikiaji wa rasilimali na maendeleo binafsi ya kila mwanajumuiya " amesema Prof.Karugila.
Naye Dkt. Sarah Chiwamba Mratibu wa Dawati la Jinsia SUA amesema Dawati hilo limeanzishwa na kuzinduliwa kwa kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na azma yao ni kuhakikisha kuwa SUA panakuwa mahali salama kwaajili ya wanafunzi kujifunza na kufikia malengo yao pamoja na wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi.
0 Comments