Na: Calvin Gwabara – Tanga.
Wakulima wa zao la Mahindi
walioshiriki kwenye Utafiti wa jaribio la kuangalia matumizi ya wadudu rafiki
katika kupambana na viwavijeshi vamizi nchini wamefurahishwa na namna wadudu
hao walivyoweza kuwatokomeza viwavijeshi na kuahidi kuachana na matumizi ya viuatilifu
sumu endapo wadudu hao watapatikana kwa urahisi madukani.
Mtafiti Mkuu Prof. Gration Rwegasira akiwa kwenye moja ya shamba la Mkulima wilayani Kilosa |
Wakizungumza na Waandishi wa
habari Wakulima hao wamepongeza utafiti huo mzuri uliofanywa na Watafiti wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushiriakana na Mamlaka ya Afya ya Mimea
na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) katika Mikoa ya Morogoro na Tanga kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Akieleza kuhusu kile alichokiona Mkulima
Salehe Alfan Ally Mkazi wa Dumila Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro amesema
kuwa wakati watafiti hao wanaleta wadudu hao wadogo na kuwaweka shambani kwake
hakuamini kama wanaweza kutokomeza kizazi cha viwavijeshi vamizi ambao wamekuwa
wakiwakosesha mavuno pamoja na gharama kubwa wanazozitumia kununua viuatilifu
sumu vya kuwaua pasipo mafanikio.
Mkulima Salehe Alfan Ally Mkazi wa Dumila Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro akionesha sehemu ya Mahindi yake yalivyobeba bila ktumia Dawa za wadudu. |
“Mimi walipowaweka wadudu hawa wakaniambia nisipulize dawa kabisa katika
wiki ya kwanza mahindi yangu shambani yakadhoofika sana, nikawaza kupulizia
dawa walipoondoka lakini nikasema ngoja nivumilie ila baada ya wiki moja
iliyofuata mahindi yakaanza kubadirika na kuwa mazuri huku nikiendelea
kuyapatia maji na mbolea na sasa angalia shamba zima hakuna mdudu, mahindi
yamependeza na hakuna hata shina moja lililoshambuliwa, yaani viwavijeshi hakuna
kabisa, haya ni maajabu kabisa” alieleza Salehe.
Amesema watu walipowaona watafiti
shambani kwake wameondoka walimfuata kumuuliza, akawasilimulia kinachofanyika
na hali ya mahindi yake yalipoharibika wakamcheka lakini baada ya muda nao hawakuamini
wanachokiona huku wao mashamba yao pamoja na kupulizia dawa bado wadudu
wanayashambulia huku wakiomba msaada nao kupata wadudu hao ili kuokoa mazao
yao.
Nae Bw. Kasote Musa Kasote
Mkulima wa mahindi kutoka Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga amesema Wadudu hao kwa
jinsi walivyofanya kazi ni mkombozi kwa wakulima wa mahindi nchini ambao
wamekuwa wakiachwa masikini baada ya mashamba yao kuvamiwa na Viwavijeshi
vamizi tangu mwaka 2017 walipoanza kuwaona mashambani mwao.
Bw. Kasote Musa Kasote Mkulima wa mahindi kutoka Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga akiongea na Waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu namna wadudu hao rafiki walivyofanya kazi. |
“Kwakweli sasa tunaona faida ya watafiti wetu na kwa jinsi wadudu hawa
rafiki walivyofanyakazi shambani kwangu nikifika dukani nikakuta wadudu na dawa
mimi moja kwa moja nitanunua wadudu hawa rafiki maana unawaweka kisha
wanazaliana wao wenyewe na kuongezeka shambani lakini dawa lazima upige kila
baada ya muda na ni ghali sana. Wengi hatuwezi, tunaomba sasa wapatikane
madukani tuweze kuwanunua” alisema Bwana Kasote.
Aidha amesema shamba lake
liligawanywa mara mbili na upande mmoja ukawekwa wadudu hao rafiki na mwingine
haukuwekwa nikabaki napulizia dawa lakini upande ambao waliweka wadudu mazao
yapo vizuri hayajashambuliwa wakati upande anaopuliza dawa mahindi bado
yanashambuliwa.
Akizungumzia matokeo ya utafiti
huo Mtafiti mkuu wa mradi kutoka SUA Prof. Gration Rwegasira amesema kwenye
mashamba hayo waliweka wadudu aina mbili ambao ni aina ya Trichogramma mwanzae na Telenomous
remus na matokeo ya maabara na kwenye kitalu nyumba yalionesha wanaweza
kuwadhibiti viwavijeshi kwa asilimia zaidi ya 90. Vilevile katika mashamba ya wakulima wamekuta udhibiti ni kwa
zaidi ya asilimia 95 hadi 98.
Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka (SUA) Prof. Gration Rwegasira akizungumzia matokeo ya utafiti huo na namna wadudu rafiki hao wanavyofanya kazi shambani. |
Mtafiti huyo aliyebobea kwenye
visumbufu vya mimea amesema uzuri wa wadudu hao wanashambulia mayai ya
viwavijeshi vamizi kwa kuyatoboa na kutagia mayai yao humo na kwa kufanya hivyo
kunasababisha Viwavijeshi Vamizi wasianguliwe bali wadudu rafiki. Hatimaye Viwavijeshi
kutoweka shambani huku akisema muda mzuri kuweka wadudu hao ni mahindi
yakishafikisha majani matatu hadi manne baada ya kupandwa hasa mkulima mayai ya
Viwavijeshi yanapoanza kutagwa kwenye mahindi.
“Kwa hiyo sisi tunachofurahia ni
kwamba mafanikio tuliyoona kwenye maabara na vitalu nyumba ya hao wadudu rafiki
tumeyaona shambani vilevile. Mfano, mdudu rafiki aina ya Trichogramma mwanzae aliweza kushambulia asilimia mpaka 90% kwenye
kitalu nyumba na hapa amepiga hizo na zaidi lakini yule wa pili aina ya Telenomous remus anakwenda hadi asilimia
98% yani karibia anaua kila kiwavijeshi na hii sasa inatudhihirishia kuwa wakulima
wetu wanaweza kulima mahindi pasipo kupulizia sumu au viauatilifu vyenye
viambata sumu kwenye mashamba yao na wakavuna vizuri” alifafanua Prof.
Rwegasira.
Aidha akijibu maswali ya wakulima
kuhusu ni lini wadudu hao rafiki watapatikana kwenye maduka ili waweze
kuwanunua Mtafiti huo amesema baada ya kukamilisha majaribio hayo sasa wakwenda
kufuata taratibu za kusajili wadudu hao kama kiuatilifu hai na baadae taratibu
za kuwazalisha na kuwafanya wapatikane kwa wakulima nchi nzima utafanyika ili
kuleta faraja kwa wakulima hasa wa mahindi ambao wamekuwa wakiteswa na
viwavijeshi vamizi kwa miaka mingi.
Viwavijeshi Vamizi kutoka Amerika
viliingia nchini mwaka 2017 kwenye mikoa michache lakini kufikia mwaka 2019 waliripotiwa
kwenye mikoa yote ya Tanzania na kwa mujibu wa Shirika la umoja wa mataifa la
Chakula na Kilimo (FAO) Viwavijeshi Vamizi wanauwezo wa kushambulia mazao zaidi
ya 80.
0 Comments