Na: Winfrida Nicolaus
Katika kuboresha ufundishaji unaoendana na
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kupitia Mradi wa HEET kimeanza kutoa
mafunzo kwa Wakuza Mitaala wa Chuo hicho ili kuwajengea uwezo
wa uandaaji wa mitaala ya kisasa itakayoendana na wakati uliopo.
Akizungumzia mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Uboreshaji na Ukuzaji wa Mitaala SUA Dkt. Jamal Jumanne amesema chini ya Mradi wa HEET unaotekelezwa hapa Chuoni wanakusudia kuwa na Mitaala ambayo itakuwa na uwezo wa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi ikiwemo kutumia njia ya mtandao na njia ya mchanganyiko (blended).
Dkt. Jamal ameeleza kuwa kupitia mitaala ambayo
inaundwa, Chuo kitakuwa na uwezo wa
kudahili idadi kubwa ya wanafunzi ambao watakuwa na uwezo wa kujifunza katika njia rahisi ambayo
itamruhusu kusoma akiwepo sehemu yoyote mbali na kukaa darasani.
“Hivyo leo tumeanza mfululizo wa Mikutano kwa
ajili ya kuwajengea uwezo Wakuza
Mitaala (Curriculum Developers) wa Chuo chetu kutoka kila
Idara ambapo tumeanza na
Idara zilizopo chini ya Ndaki ya Kilimo Chuoni
hapa na baadaye tutaenda
kwa Shule Kuu ya Uhandisi na Teknolojia na tutamalizia kwenye Kampasi yetu ya Mizengo Pinda”,
alisema Dkt. Jamal Jumanne ambaye pia
ni Mhadhiri Chuoni hapo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dkt. Salome Maro amesema
madhumuni ya mafunzo hayo ni kuhakikisha kunakuwa na vipengele sahihi hasa katika kutoa
mafunzo kwa njia ya mtandao hivyo ni
matumaini kuwa mafunzo hayo yatawaandaa vyema wakuza mitaala kuwa na ujuzi katika kuandaa
programu zenye tija ili kukisaidia
Chuo kuwa na uwezo wa kuandaa Wahitimu wenye sifa na mahitaji ya sasa.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Dkt. Gudila
Anseli kutoka Idara ya Chakula,
Lishe na Sayansi ya Mlaji SUA amesema Mafunzo ambayo wameyapata yatawasaidia kuongeza ujuzi wa kuandaa
mitaala mizuri ambayo itawasaidia
Wanafunzi wengi zaidi kujiunga na SUA kwani mifumo hiyo itakuwa na uwezo wa kumfundisha mwanafunzi
hata akiwa eneo lolote.
Maboresho ya mitaala ikiwa ni sehemu ya mahitaji
ya muhimu katika utekelezaji wa Mradi
wa HEET, pindi yakikamilika yanaelezwa kuwa yatachagiza ongezeko la udahili kwa Wanafunzi wa
ngazi mbalimbali Chuoni hapo pamoja na kuongeza ufanisi katika ufundishaji na
ujifunzaji.
0 Comments