Na: Hadija
Zahoro
Jimbo Katoliki
la Tanga kupitia Mradi wao wa kuanzisha Shule ya Sekondari limeanzisha
ushirikiano wa awali na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) hasa katika
Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuwawezesha kupata mafunzo yatakayoifanya shule
hiyo kuwa mfano wa kuigwa nchini kwa
upande wa mafunzo kwa vitendo.
Mkuu wa
Idara ya Sayansi ya Wanyama, Ukuzaji Viumbe Maji na Nyanja za Malisho kutoka
SUA Prof. Anthony Sangeda amesema ushirikiano huo utaendelezwa ili dhana hiyo ya kilimo iweze
kufikishwa kwa vijana wadogo ambao wanaweza kuendeleza utaalamu wa kilimo
katika jamii na taifa kwa ujumla.
Prof.
Sangeda amesema kupitia Mradi huo Viongozi wa Jimbo Katoliki la Tanga wameona ni
vema wajifunze kwenye maeneo ya SUA ili waweze kujua mambo muhimu ya kufanya
wanapoanzisha sekondari yao kwani vijana wanaweza kujifunza kwa kushirikiana na
Chuo hicho.
“Kimsingi
kabisa wageni hawa wana Mradi ambao wanauanzisha katika Jimbo Katoliki la Tanga ambayo ni Sekondari ya vijana na wanapenda
iwe ya mfano kwa nchi hii kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo kilimo katika nchi
ya Tanzania kwa hiyo wameona ni vyema wajifunze kwa eneo hili la Chuo Kikuu cha
Sokojne cha Kilimo”, ameeleza Prof. Sangeda.
Kwa
upande wake Padri Gerald Theodol Kabarega kutokea Jimbo Katoliki la Tanga
amesema kuwa katika Mradi huo wa Shule, wameona ni vyema kuwa na sehemu mojawapo ya kilimo ambayo itakuwa chini ya
uangalizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo ili waweze kujifunza mambo mengi yanayohusu kilimo ambapo yatawasaidia
kupata hamu ya kujiendeleza katika
masomo ya kilimo hapo baadaye.
Ameeleza
kuwa si tu kuja na elimu ya sekondari ya kawaida pekee bali kuwe na ujuzi zaidi ya elimu
ya sekondari hivyo, wamekuja Chuoni hapo
kuongea na uongozi wa Chuo pamoja na kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji
na wanaamini kwamba wakifanya makubaliano na Chuo kuweza kusimamia katika Sekta
hiyo ya Kilimo na kuweza kuwapa wanafunzi mafunzo mbalimbali basi yataweza
kuwasaidia wao na jamii inayowazunguka.
Amesema
kuwa mara baada ya kukamilika kwa Mradi huo 2025, kutakuwa na wataalam mbalimbali
wa SUA watakaokuwa wanatembelea shuleni hapo na kuwaelekeza masuala ya kilimo
katika nyakati tofauti ambapo pia wanafunzi
watapata nafasi ya kufanya ziara Chuoni hapo ili kujifunza kivitendo zaidi.
0 Comments