Na: Calvin Gwabara - Mbarali
Serikali Wilayani Mbarali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) pamoja na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kwa jitihada zao za kusaidia kurejesha uoto wa asili kwenye
vyanzo vya maji pamoja na kufanya utafiti na kutoa matokeo ambayo yataisaidia
Serikali kufanya maamuzi sahihi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali Denis Mwila wakati akifungua warsha ya kutoa matokeo hayo. |
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Mhe. Kanali
Denis Mwila wakati akifungua warsha ya kutoa matokeo ya utafiti wa Mradi wa
usimamizi endelevu wa madakio ya maji kupitia tathimini ya kuimarisha mtiririko
wa maji kwa mazingira na utekelezaji wake katika kulinda Ukanda wa Magharibi
mwa Bahari ya Hindi na athari za shughuri za kibinadamu Tanzania (EFLOWS)
iliyofanyika Wilayani humo Mkoani Mbeya.
“Kuna athari kubwa ya
kiusalama ambayo inaonekana kuja kwa juu kwa sasa ya uharibifu wa mazingira
lakini ukiangalia kwa makini na kwa mujibu wa vitabu kadhaa nilivyosoma
inaonekana vita ya tatu ya dunia itakuwa ni vita ya maji na hii imeanza
kudhihirika kwenye maeneo mbalimbali na mfano mzuri ni eneo la mto Nile na hata
ninapopita kwenye wilaya yangu kuongea na Wananchi swala la maji ndio kilio
kikubwa” alieleza Mhe. Kanali Mwela.
Amesema matokeo hayo mazuri ya kina na kisayansi ya utafiti
ya Mradi wa EFLOWS watayapitia vizuri na kuyatumia katika kutekeleza mipango
mbalimbali ya uhifadhi kupitia mapendekezo yaliyotolewa ili kusaidia kuhifadhi
vyanzo vya maji na mazingira kwa manufaa mapana na Taifa kwa kuwa vyanzo vya
maji vilivyo nyanda za juu kusini ndivyo vinavyotegemewa kutiririsha maji yake
kwenye mto Ruaha mkuu na hatimae Bwawa la Kidatu na Mwl. Nyerere
Amesema kuwa kumekuwa na uelewa kidogo wa jamii na baadhi ya viongozi katika masuala ya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji ndio maana Serikali inapochukua hatua za kuzuia shughuli fulani za kibinadamu kwenye maeneo muhimu ya vyanzo vya maji na hifadhi huzuka malalamiko mengi ambayo chanzo chake kikubwa ni ubinafsi wa watu wachache usiojali maslahi ya watu wengi na Taifa.
“Nyanda za juu wasipotunza vyanzo vya maji na kufuata sheria
za uhifadhi wa mazingira Mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere
hautafanya kazi na hivyo kusababisha nchi kukosa umeme wa kutosha kuendesha Viwanda,
Treni ya Mwendokasi (SGR) na shughuli zingine za jamii zitakwama maana nishati hii
ni muhimu kwa kila mtu” alieleza Kanali Mwela.
Mhe. Kanali Mwela amepongeza kazi hiyo kubwa ya utafiti
iliyofanywa na SUA kwa kushirikiana na NEMC katika kufanya tathimini ya
mtiririko wa maji kwenye mto Mbarali ambao unachangia maji yake kwenye Mto
Ruaha mkuu na hatimae kuelekea Bwawa la Mwl. Nyerere na kwamba matokeo hayo
yanasaidia kuonesha vizuri hali halisi ya vyanzo vya maji na mtiririko wake na
nini kifanyike.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS kutoka (SUA)
Prof. Japhet Kashaigili amesema katika kipindi cha miaka miwili ya utafiti huo
tathimini ya kina imefanyika kuangalia hali ya vyanzo vya maji vya mto Mbarali,
Afya ya Mto, Maumbile ya mto na uoto wake kupitia wataalamu waliobobea nchini
kwenye nyanja hizo kutoka taasisi mbalimbali nchini na wananchi wa maeneo hayo
hususani Jumuiya za watumia maji.
“Wakati tunakuja kutambulisha mradi tuliitana wadau wote wa
maji wa mto Mbarali na tukawaeleza malengo ya ujio wetu wa utafiti huu na wengi
wenu mlishiriki pia wakati wa utafiti wenyewe katika kipindi chote na baada ya
kukamilisha kuchakata matokeo ya yale tuliyoyaona kisayansi sasa tumeona ni
vyema kurudi tena kwenu kuwapatia mrejesho ili kwa pamoja tujue tunawezaje
kutumia matokeo hayo kwa pamoja kusaidia kulinda vyanzo vya mito yetu na
mazingira kwa faida ya Taifa” alieleza Prof. Kashaigili.
Aliongeza kuwa“ lengo la pili ni kujadili hatua za kuchukua
ili kufikia malengo ya usimamizi na mpango wa utekelezaji na kuainisha wadau,
majukumu, mpango na ushirikiano ili sote kwa pamoja tukubaliane cha kufanya na
kushiriki kikamilifu maana tunategemeana na tunakwenda na usemi uleule kuwa
ukitaka kufika mbali nenda na wenzako ila ukitaka kwenda haraka nenda peke yako
na sisi lengo ni kufika mbali hivyo lazima twende pamoja”.
Prof. Kashaigili amesema takwimu na sampuli zilikusanywa
kwenye maeneo manne waliyoyateua kupitia vigezo mbalimbali na zoezi hilo
lilifanyika wakati wa kiangazi wakati kina cha maji mtoni kiko chini na wakati
wa masika kipindi mto umejaa maji kuanzia mwanzo mwa mto katika eneo la Wilaya
ya Wanging’ombe na Mbarali ambako unaishia na kumwaga maji yake kwenye mto
Ruaha mkuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka
(NEMC) Dkt. Menan Jangu amesema Baraza linajukumu kubwa la kuhakikisha miradi
mikubwa inayoanzishwa inafikia malengo kwa kupata mahitaji yanayohitajika kwa kupitia utunzaji wa mzingira na vyanzo vya
maji.
Amesema ni wazi kuwa Mazingira, Ikolojia, bioanuai na huduma
zinazopatikana zinaendelea kupata changamoto kubwa kutokana na ongezeko la
watu, ongezeko la mahitaji na kwamba changamoto hizo zisipopatiwa ufumbuzi
rasiliamali nyingi zinaweza kutoweka hususani mtiririko wa maji ambao ni uhai
wa Wanyamapori, Binadamu na Miradi mikubwa ya uzalishaji wa nishati nchini.
“Utekelezaji wa utafiti huu ni moja ya malengo ya NEMC katika
kuhakikisha kunakuwepo na tafiti nzuri na za kina ambazo zinafanywa nchini
katika eneo la mazingira ili kupata matokeo na suluhu za kisayansi ambazo
zitasaidia kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji pamoja na mbinu za kurejesha
uhalisia kwenye meneo ambayo yameathiriwa na shughuli za kibinadamu au majanga
ya asili” alieleza Dkt. Jangu.
Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira amesema matokeo ya utafiti huo
yanatoa muelekeo wa hali ilivyo na kujua kama ni bado ni muelekeo sahihi au
kuna maeneo ya kufanyiwa kazi na ndio maana kwenye eneo la utafiti NEMC
inafanya kazi na wadau pamoja na taasisi zingine kama ilivyo kwenye mradi huu
kati ya SUA, NEMC na wadau wengine.
Mradi huu wa Utafiti unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC) na kutekelezwa katika bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la
mto Mbarali kwa ushirikiano na Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia
maji, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na
jamii, kwa ufadhili wa program ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, kupitia
michango ya nchi kumi wanachama wa Azimio la Nairobi ambapo kwa Tanzania ni kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, katika kutekeleza Mpango Mkakati wa
Kivitendo wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi chini ya uratibu wa Sekretarieti ya
Azimio la Nairobi.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS kutoka (SUA) Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya warsha hiyo. |
Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka (NEMC) Dkt. Menan Jangu akitoa salamu za NEMC. |
Dkt. Winfred Mbungu akitoa matokeo ya tathimini ya maji kwa mazingira na mtiririko wake kwenye mto Mbarali. |
0 Comments