Na: Farida Mkongwe
Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu na machapisho mbalimbali yanayopatikana katika Maktaba zilizopo nchini ikiwemo Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo ili kuweza kupata uelewa, maarifa na taarifa sahihi zinazotolewa na watafiti kupitia machapisho hayo.
Wito huo umetolewa na Mkutubi kutoka Kurugenzi ya Maktaba ya Sokoine ya Kilimo Alex Bahame Alphonce Agost 2, 2023 wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane mjini Morogoro.
Bw. Alphonce amesema machapisho yaliyopo katika Maktaba hiyo yana uwezo mkubwa wa kuwasaidia wakulima na wafugaji kuweza kulima na kufuga kwa tija kwa kutumia Kitengo kinachoitwa Mkulima collection ambacho kina machapisho ya tafiti zilizochakatwa kwa lugha nyepesi ya Kiswahili.
"Zipo tafiti nyingi zilizofanyika lakini zile tafiti zimefanyika kwa lugha ya kiingereza ile ni lugha ngeni wengine hawawezi kuelewa kwa hiyo sisi tunalo jukumu la kuchukua zile taarifa na kuzichakata kwa lugha nyepesi ambapo mkulima wa kawaida kabisa anaweza kusoma na kuelewa”, amesema Mkutubi huyo.
Amesema kuwa Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo ina mchango mkubwa sana wa kufikisha maarifa kwa jamii “kuna watu wana maarifa ambao ni vigumu kukutana nao na kukupatia maarifa walioyonayo lakini kupitia Maktaba yetu wananufaika na maarifa hayo”, amesema Bw. Alphonce.
0 Comments