Na Winfrida Nicolaus
Hospitali ya Rufaa ya Wanyama iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imekuja na huduma mbalimbali za Matibabu ya Magonjwa yote yanayoathiri wanyama hasa Magonjwa sugu ambayo yanashindikana kutibiwa katika Kliniki mbalimbali nchini.
Amebainisha hayo Prof. Mshiriki kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya Claudius Luziga Agosi 1, 2023 kwenye siku ya kwanza ya Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mjini Morogoro wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu huduma zinazotolewa na hospital hiyo.
Prof. Luziga amesema hospitali hiyo inatoa huduma za juu zaidi ikiwemo huduma ya X-ray ambayo ni ya kidigitali ambayo inawezesha upatikanaji wa tiba sahihi, uboreshaji wa wanyama ikiwemo uhimilishaji na huduma kama Utra Sound ili kutambua matatizo katika uzazi kwa Wanyama na Magonjwa yaliyopo ndani yasiyoonekana kwa macho lakini pia wanafanya upasuaji mkubwa ambao hauwezi kufanyika katika kliniki ndogo ndogo.
Amesema mbali na huduma hizo wanatoa pia Mafunzo ya namna bora ya utunzaji wa Wanyama ikiwemo kuwapatia chanjo, dawa za minyoo, namna ya kuwaogesha dhidi ya viroboto, kupe, chawa na wadudu wengine ambao wapo kwenye ngozi kwa wanyama mfano Mbwa na Paka.
“Huduma zote hizo tunazitoa kwa wale Wanyama ambao huwa wanaletwa katika Hospitali yetu ya Rufaa na wakati mwingine tunawafuata kule kwenye maeneo yao pale ambapo tunaletewa taarifa labda wanyama wanakufa wengi tunatuma wataalamu wetu wanaenda huko kwaajili ya kutoa huduma hivyo tuko kwenye Maonesho haya ya nanenane ili kuwafashamisha wakulima huduma zetu lakini pia tunatoa elimu”, amesema Prof. Luziga.
Maonesho hayo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki inayoundwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na wenyeji wake Morogoro kwa mwaka huu 2023 yamebeba kauli mbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.
0 Comments