Kituo cha Kusini mwa Afrika cha Uchunguzi wa Magonjwa Yanayoambukiza (SACIDS) kilichopo ndani ya Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA watoa Elimu kwa wananchi kuhusiana na Application za Simu zitakazo wasaidia kutoa taarifa kwenye Mamlaka husika na kuweza kufikiwa na wataalam kwa haraka kwa kutumika Maabara inayotembea ili kutatua changamoto kwa haraka ikiwemo ya Magonjwa ya kuambukiza.
Hayo yamebainishwa na Mhadhiri wa SUA wa Idara ya Fiziolojia, Biokemia na Famakolojia ambaye ni Mtafiti kutoka SACIDS Dkt. Edson Kinimi wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwl.Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro.
Amesema wao kama wadau katika Afya za wanyama, binadamu na mimea wapo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kwasababu wakulima walio wemgi wamekuwa wakipoteza mazao yao pamoja na mifugo na kuingia katika matatizo makubwa ya Kiuchumi na kushindwa kujikimu kimaisha hivyo wanapoweza kutoa taarifa kwa haraka itasaidia kuokoa mifugo na mazao yao.
“Kuna Mifugo kama Nguruwe, Kuku pamoja na Mbuzi ni Mifugo ambayo inakuwa kwa haraka sana ndani ya muda mfupi na ndiyo inayosaidia wakulima kupata kipato chao hivyo ikiharibika kutokana na Magonjwa hasa ambukizi kunakuwa na changamoto hasa Kiuchumi sasa kutokana na taarifa zao tunaweza kubaini Magonjwa kwa haraka kwa kushirikiana na jamii”, amesema Dkt. Kinimi.
Dkt. Kinimi ameongeza kuwa kuna Teknolojia nyingine za Kidijitali zenye uwezo wa kutoa taarifa za viashiria vya magonjwa na maafa katika jamii vilevile Maabara inayotembea ambayo inasaidia kubaini na kuchakata vinasaba vya magonjwa ya milipuko kwa haraka ili kuweza kuzuia magonjwa na athari ambazo zingejitokeza hivyo amewataka wananchi waishio Morogoro na mikoa ya karibu kufika banda la SUA kupata elimu na ili kujionea teknolojia.
0 Comments