SUAMEDIA

SUA yatoa fursa kwa Muhitimu kujiajiri moja kwa moja

 Na: Farida Mkongwe

Imeelezwa kuwa Kozi ya Shahada ya Lishe ya Binadamu pamoja na Kozi ya Shahada ya Sayansi ya Kaya na Mlaji zinatolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ni miongoni mwa kozi zinazotoa fursa kwa Muhitimu kujiajiri moja kwa moja kutokana na wanafunzi kufundishwa ubunifu wa kuviongezea thamani vifaa mbalimbali vilivyopo kwenye jamii.

                         


Hayo yameelezwa Agosti 5, 2023 na Msaidizi wa Wanataaluma Malogo Mkanwa kutoka Idara ya Lishe ya Binadamu na Sayansi ya Kaya na Mlaji iliyopo Ndaki ya Kilimo SUA wakati akizungumzia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wanafunzi wanaosoma kozi hizo katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro.

Bw. Mkanwa amesema katika maonesho hayo wameleta bidhaa mbalimbali ambazo zimebuniwa na kutengenezwa na wanafunzi wa kozi hiyo ambapo inaonesha jinsi wanafunzi hao walivyoongezea thamani vitu mbalimbali yakiwemo mapipa yaliyotumika na kugeuza makochi yenye thamani ambayo wanayauza na kujiingizia kipato.

Kwa mfano kama unavyoona hizi bidhaa zilizopo hapa haya yalikuwa ni mapipa tumetumia kama malighafi, haya mapipa mwanzoni yalikuwa yameshatumika labda yalikuwa na rangi au lami lakini baada ya kutumika yanakuwa hayana kazi sasa ili yasiwe taka yakaongezewa thamani wakabuni kwa kuyakata katika miundo tofauti na kutengeneza makochi unayoyaona, amesema Bw. Mkanwa.

Bidhaa nyingine hapo ni hizo meza zimetengenezwa na matairi ya magari ambayo yameshatumika sasa wanafunzi wakayaongezea thamani ili matairi yasichomwe moto au yasiyeyushwe au yasiwe taka, yametengenezewa meza mbalimbali na kuwekwa vifaa vingine kama nakshi kwa hiyo huwezi kukosa ajira kabisa kama umesoma hii kozi, amesisitiza Bw. Mkanwa.

Amesema pia wana vifaa vya kisasa ikiwemo mitambo ya kutengenezea bidhaa za ngozi na mshine kwa ajili ya ushonaji na ubunifu na kwamba wanatofautiana na mafundi wa mitaani kwa sababu wao wanawafundisha na kuwaelekeza wanafunzi kuwa wabunifu kwa hiyo wanakuwa wanabuni brand zao wenyewe ambazo wanatengeneza kutoka kwenye mawazo yao kutokana na utaalamu wanaoupata kutoka SUAamesema Msaidizi huyo wa Wanataaluma.

  Baadhi ya picha za ubunifu

 








Post a Comment

0 Comments