SUAMEDIA

Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA inawakaribisha wananchi kupata Mafunzo

Na Winfrida Nicolaus

Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA inawakaribisha wananchi kupata Mafunzo ya muda mrefu na  yale ya muda mfupi yanayotolewa na Ndaki hiyo ikiwemo mafunzo ya Lugha za Kienyeji na Kimataifa, maswala ya Jinsia pamoja na kuwaandaa watu wanaotarajia kufanya Mitihani ya Kimataifa lengo likiwa ni kutanua uelewa wao zaidi kuwa wa Kimataifa kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.



Amesema hayo Dkt. Job Mwakapina Mhadhiri kutoka SUA katika Ndaki ya Sayansi ya Jamii na Insia, Idara ya Taaluma za Lugha wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema katika Ndaki yao kuna Idara nne, Idara ya Taaluma za Maendeleo na Mafunzo ya Mkakati, Taaluma za Lugha,  Sosholojia pamoja na Idara ya Fedha na Mipango hivyo wanatoa programu nyingi kuanzia Shahada ya Kwanza, Uzamili hadi Uzamivu katika maeneo yote yanayohusu Lugha na kwamba wanatarajia kuanza mwaka ujao wa masomo 2023/2024 ambapo wataanza kutoa Shahada ya Lugha kwenye eneo la Sanaa na Ualimu ikiwa inazingatia masomo ya Kingereza na Fasihi.

Dkt. Mwakapina amesema Ndaki yao pia ina vituo ikiwemo Kituo cha Jinsia kinachohusika katika kuwajengea uelewa wanafunzi pia jamii inayowazunguka kuhusiana na maswala ya Jinsia na kufanya Tafiti mbalimbali juu ya maswala hayo lakini pia Kozi fupi kwenye maeneo hayo ya Jinsia.

Aidha amesema Kituo kingine ni cha Lugha za Kienyeji na Kimataifa (Center of African Language and International Language) kinachopatikana Kampasi ya Solomon Mahlangu kinachohusika na kutoa Mafunzo ya muda Mfupi ya Kingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kichina lakini pia Kijerumani ambapo wanashirikiana na Chuo cha FAU kilichopo nchini Ujerumani kufundisha Lugha hiyo.

Pia Kituo chetu hiki kinafanya Tafiti katika Lugha zetu hizi za kienyeji na za Kimataifa, kutafsiri na kuhariri maandiko mbalimbali lakini pia tunaanzisha mahusiano (Collaboration) na watu binafsi, Taasisi mbalimbali duniani katika maeneo ya kufundisha Lugha na kufanya Tafiti lakini pia tunaandaa watu ambao wanatarajia kufanya mitihani ya kingereza hivyo tunawaandaa kwenda kukabiliana na mitihani hiyo, amesema Dkt. Mwakapina

Dkt. Mwakapina ameongeza kuwa kwenye Nanenane ya mwaka huu anapenda kuwakaribisha zaidi Wakulima pamoja na  watoto wao kwa kuwa anatambua wapo, kwenda kujiunga na programu mbalimbali zinazotolewa na Ndaki yao kama vile Mipango, Sera pamoja na Maendeleo vijijini hivyo wafike kwenye Maonesho hayo kwenye banda la SUA kupata maelezo zaidi ya namna ya kujiunga na kozi hizo lakini pia kile watakachoenda kujifunza ndani ya kozi.

Post a Comment

0 Comments