SUAMEDIA

SUA yatoa Elimu juu ya njia sahihi kwa kudhibiti Panya wanaoharibu mazao shambani

Na Winfrida Nicolaus

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Taasisi ya Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu  wanatoa Elimu juu ya njia sahihi ambazo ni endelevu na rafiki kwa Mazingira kwaajili ya kudhibiti Panya wanaoharibu mazao shambani.





Amesema hayo Bw. Ginethon Mhamphi Msaidizi wa Wanataaluma Kutoka Taasisi ya Udhibiti Viumbe Hai waharibifu SUA kwenye Maonesho ya Wakulima, Wavuvi na Wafugaji Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika  Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na njia rahisi na rafiki wa mazingira katika kudhibiti Panya kwenye Shamba la Mazao .


Amesema miaka ya nyuma Wakulima na watu wengine majumbani wamekuwa wakitumia Mitego na sumu kwaajili ya kuua Panya lakini SUA kupitia Taasisi ya kuzuia viumbe waharibifu wameona waangalie njia ambazo ni rafiki kwa Mazingira ambapo kwa sasa wana Teknolojia mbalimbali ambazo wanaendelea kuzifanyia Tafiti na nyingine wamekwishazifanyia Tafiti na kuona kuwa zinafaa kutumika kwenye mashamba.


Mhamphi amesema Mkulima atakapoenda kwenye banda la SUA kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki atapata Teknolojia hizo ikiwemo ya Bundi ambae ana uwezo mkubwa sana wa kula Panya ambapo anakula Panya wanne hadi kumi kwa siku moja hivyo Mkulima akiwa na Bundi watatu mpaka wanne shambani kwake wanauwezo wa kuwa walinzi wa mazao.


“Mkulima anapokuja kwenye Banda letu tutamuelekeza ni namna gani ya kumvutia Bundi ili kuweza kuishi kwenye shamba lake na aweze kupunguza kiasi kikubwa cha Panya kwenye shamba lake kikubwa ni kuondokana na Imani potofu na kumuona Bundi kuwa sawa na Wanyama wengine na kumuona kama mlinzi wa mazao yako shambani”, amesema Mhamphi.


Aidha Bw. Mhamphi amesema njia nyingine ambayo wanaendelea kuifanyia utafiti ni kufukuza Panya kwa kutumia mkojo wa Paka kwa ufanisi zaidi na bado wanaendelea na Utafiti kwa kuwa ufanisi wa awali waliona Panya wana uwezo wa kuondoka kupitia njia hiyo lakini baada ya siku kadhaa wakarejea tena kwenye Mazingira hivyo wamerudi tena Maabara kuona namna wanavyoweza kuiboresha njia hiyo ili iweze kudhibiti Panya hao ikiwezekana kutorejea kabisa.


Amesema njia zingine ni kuweka wigo ambayo hutumika zaidi kwenye shamba la Mpunga na husaidia kudhibiti Panya wasiharibu Mpunga vilevile kuzuia Panya wasizaliane na hii ni Teknolojia ambayo wameshaifanyia majaribio ya Kimaabara na kuona kuwa inafaa.


                                  
          

Post a Comment

0 Comments