SUAMEDIA

SUA kupima ubora wa Mbegu na Afya ya Mimea Bure

Na: Winfrida Nicolaus

Katika kuhakikisha Wakulima wanazalisha kwa Tija na kuondokana na wimbi la umasikini, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani imetoa wito kwa Wakulima kutembelea Banda la SUA katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki Mjini Morogoro ili waelimishwe kuhusiana na Ubora wa mbegu na Magonjwa mbalimbali ya Mimea na namna sahihi ya kukabiliana nayo.





Wito huo umetolewa na  Mtaalam wa Magonjwa ya Mimea Dkt. Hellen Kanyagha kutoka Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani Agosti 03, 2023 wakati akizungumza na SUAMEDIA kwenye Maonesho  ya nanenane Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema katika Maonesho hayo wamewaletea wananchi Maabara za Mbegu kwa ajili ya kuangalia Afya ya Mbegu na Afya ya Mimea ambapo wanaangalia ubora wa mbegu vilevile Magonjwa mbalimbali ya mimea ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa jinsi ya kukabiliana na visumbufu vya Mimea pamoja na Mbegu hivyo wananchi hasa wakulima wataweza kufahamu magonjwa yanayosumbua kwenye mimea.

Dkt. Hellen amesema Mkulima anatakiwa kufahamu magonjwa ni yapi kwa kuwa akishafahamu aina ya ugonjwa au dalili zake ni rahisi kukabiliana nao hivyo wanawakaribisha wananchi hasa wakulima kwenye Maonesho hayo kupata huduma bure kabisa ya kujifunza Magonjwa mbalimbali ya Mimea pamoja na maswala yote yahusuyo Mbegu kwa ujumla.

“Mbegu bora kwanza kabisa tunazingatia uotaji, ukuaji wa mbegu ambapo tunaita Viga na baadae tunazingatia utakuja kutoa mazao kiasi gani hivyo natamani sana Wakulima wengi wangetembelea kwenye banda letu ili wapate Elimu hasa kwenye ubora wa mbegu na magonjwa mbalimbali ya Mimea na ili waweze kunufaika na kuzalisha kwa tija”, ameeleza Dkt. Hellen.

Dkt. Hellen ameongeza kuwa Maabara zao ziko wazi na wapo tayari kufanya kazi na wananchi hususani Wakulima hata baada ya Maonesho hayo hivyo anawakaribisha kwenye Maabara yao ya Afya ya Mimea na Mbegu SUA Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambapo watapata huduma zote wanazohitaji.




Post a Comment

0 Comments