Na: Asifiwe Mbembela
Wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa shule ya
Sekondari Lumumba na Ben Bella kutoka
Zanzibar wameelezwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatoa programu
mbalimbali zinazoendana na Sera ya sasa ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayohusu uchumi wa bluu.
![]() |
Bi. Zahra Majili amewaambia
wanafunzi wa shule hizo kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakidhani SUA inafundisha
programu za kilimo pekee akisema Chuo hicho mbali na program za kilimo kinatoa
programu ambazo zina mahusiano ya moja kwa moja na sera ya uchumi wa bluu
inayompa nafasi ya kuajiriwa kwenye sekta mbalimbali nchini.
“Wengi mnadhani kuwa SUA
tunafundisha programu za kilimo tu lakini niwaambie kuwa kuna programu ambazo
tunafundisha zina mahusiano na uchumi wa bluu kwani uchumi huo unakamilishwa na
programu kama Sayansi ya Mazingira na Usimamizi na nyinginezo”, amesema Bi,
Zahra.
Bi. Zahra amezitaja programu ambazo
zinafundishwa SUA zenye mahusiano na uchumi wa bluu kuwa ni Shahada ya Sayansi
ya Viumbe Hai, Shahada ya Sayansi ya Misitu, Shahada ya Usimamizi na Uhifadhi
wa Wanyapori, Shahada ya Sayansi ya Mazingira na Usimamizi, Shahada ya Sayansi
ya Uzalishaji wa Viumbe Maji na Shahada ya Sayansi na Teknoljia ya Chakula.
Kwa upande wake Omari Tunga,
Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari upande wa Udahili kutoka Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo amewasihi wanafunzi hao kuanza kujiandaa kujiunga na SUA
kwani idadi ya udahili kuanzia mwaka huu unakusudia kuongezeka kufikia wadahiliwa
zaidi ya 8,000.
Suhaylla Hamis Juma mwanafunzi
mhitimu wa SUA katika Programu ya Elimu ya Viumbe Hai wa Majini na mwajiriwa
katika Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Bluu akiongea na Kitengo cha Mawasiliano na
Masoko amesema kupitia uzoefu ambao ameupata kazini amebaini kwamba mbali na
programu ambayo amesoma kuna programu nyingine zinazofundishwa SUA ambazo zina
mahusiano na Wizara hiyo na inaendana na sera ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kupitia baadhi ya wafanyakazi wanaoshiriki Maonesho ya Elimu ya Juu kinaendelea
na mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali za sekondari zilizopo hapa Zanzibar
kwa lengo la kukitambulisha Chuo hicho pamoja na kueleza programu
zinazofundishwa Chuoni hapo.
0 Comments