Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa HEET kinapanga kuanzisha jumla ya kozi (program) mpya za Shahada 32 ambapo timu ya Wanataaluma 32 ambao watahusika na zoezi la kukusanya maoni kuhusu Mitaala mipya ya kozi hizo imekutana kwa lengo la kujadiliana na kushirikishana ufahamu kuhusu yaliyopo kwenye dodoso litakalotumika katika kukamilisha zoezi hilo.
Akizungumza na SUAMEDIA Agosti 10, 2023 Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Uboreshaji na Ukuzaji wa Mitaala SUA Dkt. Jamal Jumanne amesema Chuo kinatarajia kuanzisha Shahada za Juu 20 na Shahada za Awali 12 katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe na Kozi 3 za Astashahada katika Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo Katavi.
“Kama tunavyofahamu katika
zoezi hili kuna mitaala mingine itafutwa, kuna mingine itaunganishwa na kuna mitaala
ambayo itapewa brand tofauti lakini
pia kuna mitaala mipya ambayo itaanzishwa kwa hiyo zoezi la leo lilikuwa ni
maalum kwa ajili ya mitaala ambayo Chuo kimeridhia kuanzisha”, amesema Dkt.
Jamal.
Akizungumzia lengo la
kuwakutanisha Wanataaluma hao Dkt. Jamal amesema ni kujadili na kuwajengea
uelewa kuhusu dodoso litakalotumika katika kukusanya taarifa muhimu ambazo
zitakusanywa kwa njia ya Mtandao kupitia Jukwaa (Platform) ya Serikali ya Serikali Mtandao yaani e-Government Authoriy (eGA)
“Hii timu iliyokuwepo hapa ni
timu itakayofanya zoezi ambalo kitalaamu tunaliita Market Survey kwenda kuuliza potential employer na potential applicants
yaani wale wanaotarajia kuajiri na wale wanaotarajia kuomba kusoma kozi zetu watoe maoni yao juu ya hizi program ambazo tunazianzisha kwamba ni maarifa na ujuzi (skills) gani yaingizwe na yaboreshwe kwenye hizi program mpya”, amesema Dkt. Jamal.
Nao baadhi ya Wanataaluma
walioshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Dkt. Prisila Mkenda Mhadhiri kutoka
Idara ya Sayansi ya Viumbe Hai na Dkt. Nichodamus Mwasakilali Mhadhiri Idara ya
Taaluma za Lugha wamesema wamenufaika na zoezi hilo la kuwapitisha kwenye dodoso
litakalotumika kukusanya taarifa hizo.
“Tumenufaika na zoezi hili la
kutujengea uelewa wa dodoso hili la ukusanyaji wa taarifa mbalimbali na
mahitaji ya hizi Shahada mpya ambazo tunazianzisha huko sokoni, sasa ili kutambua soko letu ni
lipi na waajiri pamoja na wanafunzi wanaotarajia kujiunga wanataka nini,
tumeelekezana, tumejadili na kuboresha dodoso hili hivyo naamini kazi itakuwa
nzuri”, amesema Dkt. Mwasakilali.
0 Comments