SUAMEDIA

Wanafunzi wanaosoma kilimo Wilbalda watembelea SUA, wasifu elimu waliyoipata

 

Na: Winfrida Nicolaus

Wanafunzi wa Kidato cha Tatu wanaosoma somo la Kilimo kutoka Shule ya Sekondari Wilbalda iliyopo Kabuku mkoani Tanga wametembelea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kuona na kujifunza kwa vitendo kuhusiana na Kilimo ili iwe rahisi kwao kuelewa zaidi kile wanachojifunza darasani na baadae kukifanyia kazi katika jamii inayowazunguka.




Amebainisha hayo Vincent John Mwalimu wa somo la Kilimo katika shule hiyo wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusiana na lengo la kutembelea SUA kwa wanafunzi wanaosoma somo hilo.

Amesema kimsingi kwa shule yao somo la Kilimo ni la hiari hivyo wameona ni vyema kwa wanafunzi waliochagua somo hilo kutumia Chuo cha SUA ambacho kinahusika na Kilimo ili kulielewa somo la kilimo na kulifurahia zaidi na jambo kubwa ambalo walipenda kujifunza ni kuhusiana na Wanyama pamoja na Mimea ya aina tofauti hivyo wamepata elimu ya kutosha zaidi ya ile ambayo waliitarajia.

“Tumeweza kujifunza ufugaji wa Nguruwe kuanzia kuzaliwa kwake mpaka ukuaji wake, ufugaji wa Sungura na aina zake ambazo mfugaji anaweza akawafuga na kuwa na uchumu mzuri vile vile tumepata bahati ya kujifunza Uzalishaji wa Samaki huko sasa ndio tumejifunza mambo mengi kuanzia Samaki anapotaga mayai mpaka kufika sokoni”, amesema Vicent

“Lakini pia tumepata Elimu juu ya Uzalishaji wa mbogamboga na matunda ya aina mbalimbali hapa SUA na tunaamini bado tutaendelea kuja kutembelea SUA kwa sababu wanafunzi wamejifunza vizuri sana hasa kwa kuona hivyo imekuwa rahisi kwao kuelewa”, ameongeza Mwalimu huyo.

Aidha Mwl. Vicent amesema SUA imewapa wanafunzi wao mwangaza na kurejea shuleni kwao Wilbalda tayari wakiwa wamejaa Ujuzi na maarifa kuhusu somo la Kilimo na anaamini wanafunzi hao wataenda kuwa mabalozi wazuri kuhusiana na Chuo hicho kwa wanafunzi wenzao wa Kidato cha kwanza na cha pili ambao watakuwa Kidato cha tatu kwa mwaka ujao na ule unaofuata kulichagua somo hilo.

Kwa upande wake mwanafunzi Blessing Haruna amesema kufika kwao SUA kwa ajili ya kuona na kupata Elimu kuhusiana na Kilimo kumekuwa wa manufaa makubwa kwa kuwa wamejifunza mambo mbalimbali na kuwapa mwangaza wa kile wanachojifunza darasani ambapo wameongeza Maarifa ya kutosha hivyo anaishauri jamii hasa shule tofauti nchini kutembelea SUA ili kuongeza Elimu na maarifa katika Kilimo.

Naye mwanafunzi Collins Shirima amesema kujifunza sio kukaa darasani pekee bali kuona na kufanya kazi katika jamii inayokuzunguka hivyo SUA ni Moja ya eneo ambalo ni maalum na linalofaa kujifunzia kwa vitendo hasa maswala ya Kilimo na ufugaji ambapo wao wameweza kujifunza kwa kuona na itawasaidia kuwa Bora katika somo la Kilimo ambalo wanalisoma.

“Naomba niwashauri tu vijana wenzangu kuitumia SUA kama fursa kwa kuwa inawafunza ili wapate Elimu ya kwenda kufanya vitu mbalimbali katika jamii, na zaidi ya hapo inawafunza wanafunzi kutotegemea kuajiriwa pekee kwani wanaweza kujiajiri na kuajiri wengine kwa kuwa Kilimo ni ajira kamili”, amesema Shirima.

Post a Comment

0 Comments