SUAMEDIA

Maonesho ya Nanenane yaanza, Mhe. Pinda atembelea Banda la SUA

Na: Farida Mkongwe

Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda ametembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Pinda ameweza  kupata maelezo mbalimbali kuhusu shughuli zinazofanywa na Chuo hicho.

                     

 

Akiwa kwenye Banda la Idara ya Mashamba ya Mafunzo Kitengo cha Ukuzaji wa Viumbe Maji Mhe. Pinda amepata maelezo ya namna ya kufuga samaki aina ya Sato na Kambale  kutoka kwa Afisa Mafunzo wa idara hiyo Bi. Stella Genge ambapo amesema samaki hao ndio rahisi kufugika hapa nchini na kwamba tafiti bado zinaendelea kuhusu aina nyingine ya samaki wanaofaa kufugwa na kuwawezesha wafugaji kupata faida.

Aidha akiwa kwenye Banda la Idara ya Sayansi ya Wanyama, Nyanda za Malisho na Viumbe Maji, Waziri Mkuu Mstaafu amepata maelezo kuhusu teknolojia mpya ya kisasa ya kuzalisha malisho ambayo inatumia nafaka na jamii ya mikunde na kwamba faida ya teknlolojia hiyo ni kuwa haitumii udongo ambapo mbegu umwagiliwa maji na ndani ya siku saba malisho yanakuwa tayari.

Afisa Mifugo Mwandamizi kutoka Idara hiyo William Hoza amesema teknolojia hiyo pia inawafaa sana watu wanaoishi mjini ambao wanakabiliwa na changamoto ya nafasi kwa sababu inatumia nafasi kidogo kuzalisha malisho ya kutosha.

Wakiwa kwenye Banda la Taasisi ya Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda alifafanua kuhusu panya buku wanaotumika kugundua mabomu ya ardhini na kusema kuwa panya hao pia wamepata mafunzo ya namna ya kugundua nyara za Serikali  ambazo zinatoroshwa nje ya nchi.

Sasa hivi tumewafundisha hawa panya jinsi ya kugundua nyara mbalimbali za Taifa ambazo zimekuwa zinatoroshwa, kwa hiyo tumeshafanya majaribio na wenzetu wa Bandari ya Dar es salaam na wameonesha umahiri mkubwa sana kwa hiyo watu wanaotorosha meno ya tembo, meno ya faru na nyara nyingine za Serikali hawa panya wanakwenda kufanya kazi nzuri, amesema Prof. Chibunda.

Prof. Chibunda amemueleza Mhe. Pinda kuwa kwa sasa SUA ipo kwenye ushirikiano na nchi ya Uturuki kuwafundisha panya hao kwa ajili ya majanga hasa wakati wa matetemeko ya ardhi kwa sababu panya hao wakivalishwa kamera wana uwezo wa kupita sehemu ambazo mbwa hawawezi kupita na kuweza kugundua kama kuna majeruhi au manusura hivyo watakuwa ni msaada mkubwa.

Lakini kwa Tanzania panya hawa wanaweza kutumika mfano kwenye migodi wachimbaji wetu wadogo wadogo mara nyingi wamekuwa wakilipukiwa na migodi na inakuwa ni vigumu sana kujua kama wachimbaji hao wako hai au wamefariki, kwa hiyo hawa panya wanaenda kutatua tatizo hilo, amesema Prof. Chibunda.

Maonesho hayo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki inayoundwa na Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na wenyeji Morogoro kwa mwaka huu 2023 yamebeba kauli mbiu isemayo Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula.

 

 






 

Post a Comment

0 Comments