Na Winfrida Nicolaus
Ubalozi wa Japani nchini Tanzania umekabidhi Vitabu 61 (Sitini na moja) vyenye lugha ya Kingereza kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA lengo likiwa ni kuwasaidia Watafiti, Wasomi na Wanafunzi kukuza uelewa katika kuchangia maendeleo ya Rasilimali watu.
Akikabidhi vitabu hivyo Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa mapema tarehe 27/07/2023 amekabidhi vitabu hivyo kwa Menejimenti ya SUA katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro na kusema kuwa vitabu hivyo vinahusisha mada mbalimbali ikiwemo Kilimo na Teknolojia, Siasa, Uchumi, Jamii na Utamaduni wa Japani.
Aidha Mhe: Balozi Misawa amesema Japan inaamini SUA ni moja ya Vyuo Vikuu vya matumaini nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wao wa muda mrefu hivyo kupitia vitabu hivyo wataendelea kupata wanafunzi kutoka chuoni hapo vilevile nchi yao inaweza kushirikiana vema na SUA hasa katika Sekta ya Kilimo, Usindikaji wa vyakula kama moja ya sehemu ya kilimo ambayo hata wao wamekuwa wakifanya.
‘‘Tumetoa Vitabu kwa Taasisi zaidi ya 1100 kote ulimwenguni kwa Tanzania Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni Chuo Kikuu cha nne kupatiwa vitabu baada ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Dodoma (UDOM) nikiwa kama shahidi Ubalozi wa Japani nchini Tanzania tuliamua kupendekeza SUA kama mwenyeji kwasababu ya ushirikiano wa karibu na wa muda mrefu tulionao baina yetu’’ amesema Mhe. Yasushi Misawa.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa Ziara ya Balozi huyo wa Japani SUA ni katika kuendeleza mashirikiano baina yao ambayo yamekuwepo tangu miaka ya 70 na yamekuwa yakiendelea kuimarika siku hadi siku ambapo Japani imekuwa mfadhili katika Miradi mbalimbali chuoni hapo.
Aidha Prof. Chibunda amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi ya Tanzania na nchi za kigeni na kusema kuwa Japan imekuwa ikikipatia SUA nafasi kwa Watafiti na Wanataaluma wao kufanya kazi pamoja na Watafiti na Wanataaluma wa Kijapani, kuwasomesha ambapo hivi karibuni kutakuwa na wanataaluma watatu watakaoenda kuanza masomo yao ya Uzamivu katika vyuo mbalimbali nchini Japan.
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo amesema kukabidhiwa vitabu hivyo na Ubalozi wa Japani ni safari ambayo inakamilisha ushirikiano wa muda mrefu baina ya SUA na nchi hiyo hasa upande wa Tafiti ambapo kwasasa wana Miradi zaidi ya sita ambayo wameshirikiana .
‘‘Katika ushirikiano huo kuna maeneo makubwa ambayo tumesababisha matokeo makubwa ikiwemo Nyanda za Juu Kusini Mbinga ambapo tulianzisha Kilimo kwenye Milima ya Matengo ambapo SUA ilikuwepo kwa muda mrefu na kusaidia katika kuzuia mmomonyoko wa Ardhi lakini pia kwa Morogoro Mradi mkubwa ulioleta matokeo makubwa ni Kilimo cha zao la Vanila na ubora wa zao hilo ni kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanasayansi wa Japani’’, amesema Prof. Karimuribo.
Akielezea umuhimu wa vitabu hivyo kupokelewa chuoni hapo Kaimu Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo SUA Prof. Wulystan Mtega amesema vitabu walivyokabidhiwa kwa kiasi kikubwa vinahusu Japani lakini katika fani tofautitofauti ikiwemo Kilimo, Siasa, Uchumi na Teknolojia ambapo watumiaji wao wa Maktaba wanahitaji machapisho mbalimbali kama hayo hivyo vitawasaidia katika kuelewa mbinu mbalimbali ambazo Japan wamekuwa wakizitumia katika kujikwamua kiuchumi.
0 Comments