SUAMEDIA

Fanyeni tafiti kubaini changamoto zilizopo kwenye udongo - Mhe. Pinda

 Na: Farida Mkongwe

Taasisi zinazofanya tafiti nchini ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) zimetakiwa kushirikiana katika kubaini na kutatua changamoto zilizopo kwenye udongo ili kuwasaidia wakulima waweze kulima kwa tija na kuendeleza sekta ya kilimo nchini.


Kauli hiyo imetolewa Agosti 1, 2023 na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda wakati akifungua rasmi Maonesho ya 30 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwl.Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro.

Mhe. Pinda amesema Rais Samia ameahidi kuwa ataendelea kuongeza bajeti ya kilimo, mifugo pamoja na uvuvi na kutolea mfano wa bajeti ya mwaka  2022/2023 ambayo iliongezeka hadi kufikia bilioni 751 .1 kutoka sh. bilioni 294.2 kwa mwaka 2021/2022 ambapo pia bajeti ya mwaka 2023/2024 iliongezeka na kufikia bilioni 970.8 hali inayoonesha dhamira ya dhati ya Rais kutaka mabadiliko chanya katika kilimo.

“Dhamira hii ya Mama ili ifanikiwe ni lazima tuanzie kwenye udongo, udongo unatakiwa uwe na afya, upimwe, uwekwe mbolea nadhani katika hili mama amelenga jambo zuri sana na sasa amesema tutumie muda kuongeza matumizi ya matrekta katika kilimo, na hapo sasa inaweza kutusaidia kuvuta vijana na hata sisi akina babu tuingie kwenye kilimo”, amesema Waziri Mkuu huyo Mstaafu.

Ameongeza kuwa suala kubwa zaidi ni upatikanaji wa huduma za ugani na kuimarisha tafiti “sasa bahati nzuri katika Kanda yenu hii SUA wanafanya tafiti, mna kituo cha utafiti TARI na wenyewe ni watafiti wazuri tu kwa hiyo mimi ningeshauri mshirikiane taasisi hizi na nyingine ambazo mnaweza mkazibaini alafu tuone namna ya kuzitumia fedha hizi ambazo Mama amezielekeza kwenye tafiti ili tuweze kuona ni nini kimekosekana kwenye udongo na kuangalia tufanye nini ili tuweze kufanya vizuri zaidi”, amesema Mh. Pinda.

Kabla ya hotuba yake ya ufunguzi Mh. Pinda alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo kwenye maonesho hayo ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi likiwemo banda la SUA na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Chuo hicho likiwemo suala la upimaji wa udongo linalofanywa kupitia Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia. 

Post a Comment

0 Comments