SUAMEDIA

Wanafunzi Kisutu waipongeza SUA


Na Farida Mkongwe

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kisutu ya jijini Dar Es Salaam wamekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kutoa kozi mbalimbali ambazo wanazifundisha kivitendo zaidi na hivyo kuwawezesha wahitimu wa Chuo hicho kuweza kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe.




Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisutu wakisoma kozi zinazotolewa SUA kupitia vipeperushi.
                                                              Picha na Asifiwe Mbembela.

Wakizungumza na SUAMEDIA Julai 19, 2023 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam ambako yanafanyika Maonesho ya Vyuo Vikuu Zulekha Nioka, Zulfa Masudi na Mariam Athumani wamesema wao wakiwa wanavyuo watarajiwa wamefurahishwa sana na maelezo waliyoyapata katika banda la SUA na kwamba watasoma kwa bidii ili waweze kufaulu vizuri na kusoma Chuo cha SUA.

“Chuo cha SUA ni Chuo kizuri sana kimetuelekeza vitu vingi sana kwa leo tumeweza kujua kozi mbalimbali na kwamba tukitoka hapa tujue tunaelekea kwenye kozi gani ili kufikia malengo, kwa kweli maelekezo tuliyopewa yanamvutia mwanafunzi kusoma kwa bidii ili afaulu maana wametwambia ili upate kozi nzuri ni lazima ufaulu vizuri”, amesema mmoja wa wanafunzi hao.

Kwa upande wake mwalimu Avitus Mjwauzi ambaye aliongozana na wanafunzi hao amesema malengo ya kufika katika banda la SUA ni kupata ufahamu kuhusu kozi zinazotolewa na Chuo hicho kama njia mojawapo ya kuwapa motisha wanafunzi wao waweze kujiandaa na masomo ya vyuo vikuu.

“Wito wangu kwa wanafunzi ni wafanye juu chini waweze kujiunga na Chuo cha SUA kwa sababu ni Chuo ambacho kinahusu kozi nyingi za sayansi na ni Chuo ambacho ukitoka pale unaweza kujiajiri ama unaajirika kiurahisi nina mifano mingi ya marafiki zangu ambao wamesoma SUA na sasa wana maisha mazuri”, amesema Mwalimu Mjwauzi.

Akizungumza na wanafunzi hao Afisa Udahili kutoka SUA Bi. Grace Kihombo amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa kuwa hakuna njia ya mkato ya kufaulu zaidi ya kusoma.


Baadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Afisa Udahili wa SUA (ambaye hayupo pichani).
                                                        Picha na Asifiwe Mbembela.


Afisa Udahili wa SUA Bi. Grace Kihombo akiwaeleza wanafunzi kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na SUA. Picha na Asifiwe Mbembela. 



Post a Comment

0 Comments