SUAMEDIA

Fika banda la SUA ufanye usajili na kupata elimu ya bidhaa zinazozalishwa

 

Na Farida Mkongwe

Wakazi wa mkoa wa Dar Es Salaam na maeneo ya jirani wametakiwa kufika Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA lililopo katika viwanja vya Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar Es Salaam ili kupata elimu na kujionea bidhaa zinazozalishwa na SUA ambazo ni matokeo ya tafiti mbalimbali.



Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (SUA) Dkt. Devotha Mosha
 akiwa kwenye banda la SUA katika Maonesho ya Vyuo Vikuu jijini Dar Es Salaam. 
Picha na Asifiwe Mbembela.

Akizungumza na SUAMEDIA Julai 17, 2023 katika viwanja hivyo Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza Dkt. Devotha Mosha amesema pamoja na usajili wa wanafunzi wanaojiunga na Vyuo vikuu unaofanyika katika banda hilo pia watu  watakaofika watapata elimu kuhusiana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na watafiti wa SUA kwa kushirikiana na watafiti wengine wa ndani na nje ya nchi.

“Kuna mazao mbalimbali, kuna miche ya matunda kama miembe, mipapai, michungwa, mipera, miparachichi, pia kuna mboga za aina mbalimbali, kuna mazao ya nyuki kama asali pamoja na mizinga ya kisasa kwa ajili ya ufugaji wa nyuki, vile vile kuna miradi ambayo imeleta mazao ya dawa mbalimbali za asili ambazo zinasaidia kutibu binadamu na mifugo, nasisitiza watu wafike kwa wingi waweze kunufaika na SUA “, amesema Dkt. Devotha

Bidhaa nyingine zilizopo katika maonesho hayo ni pamoja na Maabara inayotembea ambayo inayotoa huduma katika maeneo mbalimbali na Kitengo cha Kudhibiti Viumbe hai waharibifu kama panya na wengine.

Kwa upande wake Afisa Mahusiano na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA Bi. Suzana Magobeko amesema katika banda lao la SUA wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanatoa huduma bora na hasa kwa wahitimu wa kidato cha sita wa 2023 na wale waliomaliza miaka ya nyuma.

“Kwa kweli hiki Chuo kimekuwa ni Chuo cha pekee kabisa kutokana na mafunzo ambayo tunatoa, wanafunzi muda mwingi wanafanya mafunzo kwa vitendo na hii imepelekea kuwatofautisha na wanafunzi wengine wanaohitimu katika vyuo vingine Tanzania, kwani tunawaandaa kwa ajili ya kujiajiri na kinachofurahisha zaidi ni kuwa wanafunzi wanaohitimu SUA wamekuwa ni msaada wa ajira kwa wanafunzi wanaohitimu katika vyuo vingine hapa nchini”, amesema Bi. Suzana.

Maonesho hayo ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yameanza rasmi Julai 17, 2023 na yatamalizika Julai 22,2023, yakibebwa na kauli mbiu ya "Kukuza Ujuzi Nchini Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani".

Post a Comment

0 Comments