SUAMEDIA

Maabara inayotembea SUA yawa msaada wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko

 

Na Farida  Mkongwe

Imeelezwa kuwa Maabara inayotembea iliyopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambayo yangeweza kuleta madhara kwa binadamu, wanyama na mifugo.



Mhadhiri wa SUA Dkt. Edson Kinimi akizungumzia mafanikio ya Maabara inayotembea 
akiwa banda la SUA lililopo viwanja vya Maonesho ya Vyuo Vikuu Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam

Hayo yameelezwa na Mhadhiri wa SUA kutoka Idara ya Fiziolojia, Biokemia na Famakolojia Dkt. Edson Kinimi ambaye yupo kwenye Kituo Mahiri cha Utafiti wa Magonjwa ya Mlipuko (SACIDS) wakati akizungumza na SUAMEDIA katika viwanja vya Maonesho ya Vyuo Vikuu  yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Es Salaam.

Dkt. Kinimi amesema Maabara hiyo inayotembea imeweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na wameileta kwenye maonesho hayo ili watanzania waweze kuona namna inavyofanya kazi na kupata mawasiliano ili pindi linapotokea tatizo kwenye jamii wajue namna watakavyowasiliana na kutatua changamoto katika hatua za awali hasa kwenye kipindi cha mvua na sehemu zenye miundombinu korofi ya barabara ambazo hazifikiki kwa urahisi.

“Tumekuja na teknolojia mpya ya Maabara inayotembea ambayo inatusaidia kubaini na kuchakata vinasaba vya magonjwa ya milipuko kwa haraka sana maana ukiweza kutambua vinasaba ndani ya siku saba kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia magonjwa hayo na athari ambazo zingejitokeza na gharama za kudhibiti ugonjwa zinapungua kwa kiasi kikubwa”, amesema Dkt. Kinimi.

Amesema Maabara hiyo ina vifaa vyenye uwezo mkubwa na teknlojia ambazo zinaweza kutambua vinasaba kwa haraka sana na kuwa na majibu ya uhakika kwenye sehemu ambayo mlipuko wa magonjwa umetokea.

Amefafanua kuwa taarifa nyingi huwa wanazipata kupitia mfumo wa Afya Data ambao kazi yake kubwa ni kuripoti viashiria vya magonjwa kutoka kwa jamii ambapo jamii husika wakipata au kuona dalili mbalimbali za magonjwa wanajaza kwenye mfumo huo kisha taarifa zinaenda kwenye ngazi mbalimbali kuanzia wilaya, mkoa hadi Taifa,

“Sisi tukipata taarifa hizo tunaenda na Maabara yetu na kuchakata na tukishapata majibu tunayapeleka kwenye wizara husika na kufanyiwa kazi”, amesema Dkt. Kinimi.



Post a Comment

0 Comments