Na: Farida Mkongwe
Jamiii imetakiwa kutumia miti ya mbao ambayo haijapewa kipaumbele katika matumizi na kuacha kutumia miti inayokaribia kutoweka ili kuinusu miti hiyo iendelee kuwepo nchini kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mbonea Mweta ameiambia SUAMEDIA jijini Dar Es Salaam kuwa kwa sasa badala ya wananchi kutumia miti kama Mvule, Mninga au Mpingo ambayo inatumia muda mrefu kuanzia miaka 70 na kuendelea hadi kuvunwa wanaweza kutumia miti mbadala iliyofanyiwa utafiti na kuonekana ina ubora sawa katika matumizi yao.
“Idara
yetu ya Uhandisi Misitu na Sayansi ya Mazao ya Misitu tumefanya utafiti na kuja
na miti mingine mbadala wa miti hiyo mfano hapo zamani tumezoea kwamba ili mtu
atengeneze kinyago ni lazima atumie mpingo lakini baada ya utafiti tumebaini
wananchi wanaweza kutumia mti wa Tamarindus
Indica (Mkwaju) ambao unapatikana katika mazingira yetu katika utengenezaji
wa vinywago”, amesema Mbonea.
Akizungumzia
miti ya mbao Mbonea amesema Idara yao imeendelea kufanya tafiti zinazohusu
matumizi sahihi ya mbao kwa kuoanisha na sifa zake kwa lengo la kutunza
rasilimali za misitu nchini na kwamba miti ambayo ina thamani kubwa iwekewe
matumizi ambayo yanaendana na thamani yake.
Aidha
Mkufunzi huyo amewataka wananchi kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda
miti ili kuleta mabadiliko chanya katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wananchi
tunawahimiza upandaji wa miti, kuzuia ukataji miti ovyo lakini vile vile
kutunza rasilimali za misitu ambazo tunazo Tanzania kwa sababu moja ya madhara
ya kutokuzuiliwa au kutokupunguzwa kwa hewa ukaa katika mazingira yetu ni
uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaleta matatizo
mbalimbali hapa nchini”, amesema Mbonea.
0 Comments