SUAMEDIA

SUA kimesaini makubaliano ya awamu nyingine kwa miaka mitano na China

Na Hadija Zahoro

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesaini  makubaliano ya awamu nyingine ya miaka mitano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China yenye lengo la kuendeleza  mahusiano  katika nyanja za Utafiti, Mafunzo  pamoja na Ushauri elekezi.


Hayo ameyasema  Mratibu wa mpango  wa makubaliano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China, Prof. Deogratius  Rutatora  wakati akizungumza na SUAMEDIA  leo Tarehe 24/07/2023 mara baada ya zoezi la utiaji saini wa makubaliano hayo kufanyika katika Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo iliyopo Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine, Morogoro.

Prof. Rutatora amesema kuwa makubaliano hayo yanatoa nafasi kwa walimu wa  vyuo vikuu hivyo viwili  kuweza kukaa pamoja na kuandaa programu  zitakazosaidia maendeleo ya siku ya kilimo kwa ujumla wake ikihusisha mazao,mifugo, uvuvi, nyuki pamoja na utunzaji  endelevu wa maliasili zilizopo nchini hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kuwa makubaliano hayo yatanufaisha SUA kwa kupata ujuzi waliotumia china umeonesha kwa namna gani nchi hiyo imeweza kunasua wananchi wake kutoka kwenye umasikini.

Aidha ameongeza kuwa njia moja wapo China waliyotumia ni kwamba vyuo vikuu vya kilimo viliweza kukaa pamoja na watunza sera na wataalamu wao  na kuanza na kilimo kilicholenga wakulima wadogowadogo wa nchi yao na hatimaye kupata majaribio mazuri  yaliyoweza kutengeneza programu  ambazo zimewasaidia masikini na kufikia mahali walipo.

‘‘Lakini wao wanasisitiza kwamba wataalamu wa kilimo ni vizuri zaidi wakakaa na serikali yao kuu, serikali za mitaa ,wenye viwanda pamoja na sekta binafsi  kwani mahusiano hayo yanaweza kusaidia kuwa na mtazamo wa pamoja wa namna gani mkulima mdogo anaweza akajinasua kwenye umasikini na akawa na kilimo chenye tija  na endelevu kulingana na mazingira yake pale alipo’’ anaeleza Prof.Rutatora 

Pia, ameeleza kuwa moja ya kipengele katika makubaliano hayo kinalenga mafunzo  ambayo hayagusi tu walimu au watafiti pekee bali hata kwa wanafunzi waliopo kwa kipindi Fulani, hivyo kulingana na programu zao za mitaala zilivyo, wataruhusiwa kwenda nchini China kwa kipindi cha wiki tatu,mwezi  na hata miezi mitatu kuangalia nadharia au vitendo vinatekelezwa kwa namna gani.

Prof. Rutatora ameongeza kuwa wanachokilenga wao ni kuangalia wanafunzi wangapi na wepesi kujifunza na wao  kuweza kuandika  mapendekezo ya mradi na kuweza kuwashika mkono  ili na wao wakitoka china  waone ni wapi hawapigi hatua na hatimaye waweze kusaidia wanafunzi wenzao na kuhakikisha wanakua na uelewa wa pamoja.

Pia amesema kuna fursa kwa wanafunzi hususani wa Shahada za awali ambao wataonekana kutenda vizuri watapewa nafasi ya kujiendeleza katika ngazi ya shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu  lengo likiwa ni kuanisha vizuri  nadharia na vitendo  ili  uwezo unaotakiwa kwa mwanafunzi awe nao kuanzia  maarifa, stadi za kazi, utashi na mwelekeo wa kutenda vitu kwa pamoja.

Katika Picha










Katika video bofya hapa chini




Post a Comment

0 Comments